Yanga yavuta winga mpya | Mwanaspoti

WAKATI Yanga ikijipanga kumalizana na Singida Black Stars juu ya beki Frank Asink, kuna mwingine ameshatangulia kambi ya mabingwa hao akijifua na jana alitarajiwa kusafiri na chama hilo kwenda Kigali, Rwanda kwa ajili ya mchezo wa kirafiki na Rayon ya huko.

Hiyo ni mosi, pili ni kwa kikosi cha mabingwa wa Ligi Kuu Bara kimeondoka na wachezaji 24 ambao wameenda kujifua, huku kocha mkuu Romain Folz akiondoka na cheko kuuubwa baada ya kuwashuhudia mastaa wake wakikipiga vilivyo katika mazoezi ya siku mbili – tatu yaliyofanyika Dar.

Lakini, huku nyuma unaambiwa kwamba Yanga imeshamalizana na Singida Black Stars ikimchukua winga mzawa Edmund John na tayari ameshajisalimisha kambini na yupo katika msafara wa mabingwa hao, akijipanga kuwaonyesha Wananchi mavitu msimu ujao wa mashindano.

Edmund alikuwa Singida kuanzia msimu uliopita aliposajiliwa akitokea Geita Gold wakati ikiwa Ligi Kuu Bara.

Yanga imemsajili Edmund kwa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine mmoja, akija kujiuliza ndani ya mabingwa hao.

Edmund anaweza kucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji akitokea pembeni, akisifika kuwa na kasi na uwezo wa kufunga.

Itakumbukwa Mwanaspoti liliwahi kugusia juu ya usajili huo akiwa kwenye orodha ya mastaa wa Singida ambao Yanga ilikuwa ikiwapigia hesabu kusajiliwa dirisha hili.

Kiungo huyo tayari  ameshaanza mazoezi na Yanga yanayoendelea pale uwanja wa KMC Complex, chini ya kocha Romain Folz.

Folz amempokea Edmund kisha kufanya naye kikao kifupi kabla ya jana kuanza mazoezi kamili akiwa na wenzake wa kikosi hicho.

Winga huyo amekuwa sehemu ya msafara wa Yanga ambao wametimkia nchini Rwanda kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji wao Rayon Sports ya huko.

Kama hufahamu ni kwamba Edmund aliwahi kuhitajiwa na Simba wakati akiwa Geita, lakini Singida ikawawahi wekundu hao na kumsajili fasta.

Wachezaji wapya ambayo Yanga iliyopo kambini imeshawatangaza ni Andy Boyeli (mshambuliaji), Celestine Ecua (kiungo mshambuliaji), Abubakar Nizar ‘Ninju’ (kiungo), Abdulnassir Mohammed ‘Casemiro’ (kiungo), Offen Chikola (winga),

Balla Conte (kiungo), Lassine Kouma (kiungo), Mohamed Doumbia (kiungo) na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ (beki).