50 mbaroni wakituhumiwa kuchoma hifadhi, kufanya vurugu

Geita. Watu 50 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Geita kwa tuhuma za kuchoma hifadhi ya msitu na kufanya vurugu.

Katika taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Agosti 15, 2025 na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Adam Maro imeeleza watu hao wanadaiwa kuwashambulia maofisa misitu wanne, kuharibu mali mbalimbali za ofisi ikiwemo kuchomamoto pikipiki moja miche ya miti 50,000 iliyokuwa kwenye vitalu na miti 236,643 iliyokuwa imepandwa.

Awali, juzi inadaiwa wananchi wa Kijiji cha Lwamgasa, Kata ya Lwamgasa wilayani Geita waliandamana na kuchoma moto eneo lenye ukubwa wa hekta 213 na kuwajeruhi maofisa wanne wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kwa kile kinachodaiwa ni kupinga unyanyasaji na matukio ya ukatili wanayofanyiwa na maofisa hao.

Pia, wananchi hao wanadaiwa kuchoma moto eneo pia wananchi kuharibu miti 236,643 iliyokuwa imepandwa pamoja na kuharibi vitalu vya miti 50,000 na kubomoa majengo ya ofisi zilizopo eneo la hifadhi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa TFS Kanda ya Ziwa, Ibrantino Mgiye, amesema wananchi hao walivunja milango, kuondoa madirisha na kuondoka nayo na kuvunja baadhi ya kuta za jengo jambo ambalo ni la kihalifu.