Dar es Salaam. Mtunzi na mwimbaji wa nyimbo za hamasa za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), George Mwingira aliyetamba na wimbo wa ‘No reforms no election’, anatarajiwa kuzikwa kesho Jumamosi Agosti 16, 2025.
Mwingira maarufu ‘MC Mwingira’ alikutwa na umauti huo baada basi alilokuwa akisafiria kupata ajali maeneo ya Mikumi mkoani Morogoro, Jumapili Agosti 10, 2025. Inaeleza kuwa Mwingira alikuwa akitoka Songea kuja Dar es Salaam, kuhudhuria kesi ya mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu anayekabiliwa na mashtaka ya uhaini.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Agosti 15, 2025, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Kusini (Ruvuma, Mtwara na Lindi), Belle Ponera amesema mwili wa Mwingira umewasili Songea alfajiri ya leo ukitokea mkoani Morogoro.
“Baada ya mwili wake kufika tuliupeleka moja kwa moja mochwari, kesho tutakwenda kumzika katika makuburi ya Kijiji cha Litapwasi wilayani Songea. Kwa sababu makaburi yapo nje ya mji, tutaanza safari saa tano asubuhi, na kuzika itakuwa saa tisa alsairi.
“Kwa watakaopata na nafasi kushiriki mazishi haya, tunawaomba waje nyumbani kwa mama yake Mwingira (Matarawe) ili tuanze safari kwenda makuburini kwa pamoja,”amesema Ponera ambaye alikuwa akifanya kazi kwa ukaribu na Mwingira.
Jana Alhamisi Agosti 14, 2025 uongozi wa Chadema na familia ya Mwingira walimzungumzia msanii huyo, aliyetamba na wimbo wa ‘Tundu Lissu wapeleke mchakamchaka’ wakisema ameacha pigo kwa sababu alikuwa kijana mvumilivu, asiyekata tamaa na mwenye upendo kwa watu wote.
“Nimemfahamu Mwingira kwa muda mrefu, tangu Mwanacotide (Fulgence Mapunda-marehemu) akiwepo, amepambana sana hadi hapo alipofikia, haikuwa kazi rahisi kwake. Wakati ule kulikuwa na wasanii, lakini Mwingira alivumilia hadi kutoka na kuwa msanii mkubwa ndani ya Chadema.
“Kuna kipindi alikuwa anatunga nyimbo lakini haziwezi kusikika, si unajua kiongozi anaweza kukubania, lakini Mwingira hakukata tamaa au kujaribu kukimbia. Mwingira ametutoka akiwa msanii kiongozi wa chama, tumeumia sana,” alisema John Heche ambaye ni Makamu Mwenyekiti Chadema (bara).
Wakati Heche akieleza hayo, mmoja wa wanafamilia wa Mwingira aliyeomba jina lisitajwe, alisema ndugu yao alikuwa mtu mwenye unyenyekevu na tegemezi katika familia yao.
Kifo hicho, kimeongeza pigo kwa Chadema baada ya msanii wake huyo wa tatu kufariki dunia, baada ya Mwanacotide aliyewahi kutamba na nyimbo za “Chadema People’s Power” na “Polisi msitupige mabomu, Chadema ni Serikali ijayo.”
Mwanacotide alifariki dunia mwaka 2019, akifuatiwa na Sarah Alex aliyetamba na wimbo wa “Mwamba tuvushe” aliyefariki dunia mwaka 2022.