Azam, Yanga walimaliza kiaina sakata la Ninju

BAADA ya sintofahamu juu ya usajili wa kiungo Nizar Abubakar ‘Ninju’ kutoka JKU ya Zanzibar akijiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka mitatu, huku Azam FC ikiibuka na kudai ni mali yao, mabosi wa klabu hizo wamekutana na kulimaliza na ni rasmi sasa mchezaji huyo atacheza Jangwani.

Imeelezwa kuwa Agosti 6, 2024 Azam ilimpa kijana Ninju mkataba wa malezi, yaani wa akademi wa miaka mitatu uliotakiwa kukoma mnamo Agosti 5, 2027, kanla ghafla wakashangaa kuona akitambulishwa Yanga baada ya kuivutia timu hiyo akiwa JKU aliyokuwa akiitumikia kwa mkopo.

Wakati Yanga ilimtambulisha Julai 27 mwaka huu kuwa ni mchezaji wamemsajili akitokea JKU na ndipo mgogoro ulipoibuka kutoka Azam ikathibitisha kuwa ni mchezaji wao.

Lakini leo Agosti 18, Matajiri wa Dae es Salaam kupitia taarifa iliyotolewa na uongozi wa klabu hiyo imefikia makubaliano na Yanga kuhusu mchezaji huyo.

“Azam inampatia baraka zote mchezaji huyo na kumtakia kila la heri katika maisha mapya ya soka.Pia tunaipongeza klabu ya Yanga kwa weledi waliouonesha hadi kupata muafaka.”

Ninju ni mchezaji kiraka ambaye ana uwezo wa kucheza nafasi zote za nyuma kuanzia kiungo mkabaji, beki namba mnili, tatu na kati isipokuwa kipa.