Tanga. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeshauriwa kuendelea kutoa elimu mahsusi kwa watu wenye uziwi kuhusu namna ya kutambua alama muhimu zilizopo kwenye noti na sarafu, ili kuwasaidia kubaini fedha halali dhidi ya zile bandia zinazoweza kuingia kwenye mzunguko wa kila siku.
Ushauri huo umetolewa leo Ijumaa, Agosti 15, 2025 na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Sebastian Masanja, wakati wa mafunzo maalumu yaliyotolewa na BoT kwa watu wenye uziwi mkoani humo.
Masanja amesema kundi hilo lina haki ya kupewa elimu sahihi ya utambuzi wa fedha, sambamba na mbinu bora za utunzaji wake, kwa kuwa kuna changamoto kubwa katika jamii kuhusu namna fedha zinavyohifadhiwa visivyo, hali inayopelekea kuharibika mapema.
“Kuna baadhi ya wananchi huhifadhi fedha kwenye mazingira yasiyofaa, kama kuzifunga kwenye khanga au kuzitunza kifuani, jambo linalosababisha fedha kuharibika kutokana na joto au unyevu wa mwili. Hii huathiri alama muhimu zilizopo kwenye fedha na huweza pia kufifisha thamani yake,” amesema Masanja.
Ameongeza kuwa matendo hayo husababisha hasara kwa Serikali kutokana na gharama za uchapishaji wa fedha mpya ili kuchukua nafasi ya zile zilizoharibika mapema.

Katika kuhakikisha elimu hiyo inawafikia walengwa, Masanja ameishauri BoT kuongeza kasi na ubunifu katika namna ya kufikisha elimu hiyo kwa watu wenye ulemavu wa kusikia, kwa kutumia lugha ya alama na mifumo inayowezesha mawasiliano yao kuwa rahisi na yenye tija.
Mafunzo hayo yamekuwa sehemu ya juhudi za Benki Kuu kuhakikisha makundi yote ya kijamii yanashiriki kikamilifu katika ulinzi wa mfumo wa fedha wa nchi, sambamba na uelewa wa majukumu ya BoT katika kulinda thamani ya fedha na kudhibiti mzunguko wa fedha bandia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Chama cha Watu wenye Viziwi Mkoa wa Tanga, David Nyange amekiri kuwepo changamoto ya baadhi ya watu wenye uziwi kukamatwa kutokana na kukutwa na fedha ambazo sio halali na yote ni kutokana na kukosa elimu ya kuzitambua.
Amesema katika ufuatiliaji wake fedha hizo hupatikana kwenye maeneo yenye mzunguko mkubwa wa fedha hasa kwenye vituo vya mabasi, sokoni na maeneo mengine yenye watu wengi, hivyo wanaendelea kupeana elimi kuzitambua.

Nyange amesema elimu waliopewa wataipeleka na kwenye makundi mengine lengo ni kusambaza utaalamu huo wa kutambua fedha fedha ambazo ni halali na zile ambazo sio halali.
Ofisa Uhusiano kutoka BoT, George Helahela amesema zoezi la kutoa elimu ya kutambua fedha halali na zile ambazo sio halali kwenye mzungumko linaendelea, na wanategemea kukutana na makundi mengi zaidi.

Ameongeza kuwa Tanga ni miongoni ya mikoa ambayo wamefanya mafunzo hayo ila ipo mingine kadhaa tayari na lengo kubwa ni kuwafikia makundi hayo maalumu ambayo sio rahisi kutambua mambo mbalimbali ya kifedha bila kupatiwa elimu.
Amesema sio mara ya kwanza kwa makundi hayo kupewa elimu ya kutambua alama ambazo ambazo zipo kwenye fedha, ila ni zoezi endelevu ambalo pia limeonyesha mafanikio kwa wahusika kueleza kupata uelewa.
Mmoja wa watu wenye Uziwi mkoani Tanga Upendo Dafa amesema mafunzo hayo ya BoT yamewasaidia kutambua alama muhimu ambazo zinapatikana kwenye noti mbalimbali,ambapo awali wengine walikuwa hawazitambui.

Ameomba elimu kama hiyo iwe endelevu kwa makundi tofauti kwa wilaya zote kwani wapo wenye uziwi na wanafanyabiashara hivyo ni muhimu wapatiwe elimu kama hiyo ambayo itaweza kusaidia wabaini fedha ambazo sio halali.
Elimu hiyo imetolewa kwa makundi ya Watu Wenye Uziwi kutoka wilaya ya Mkinga, Pangani na Tanga ili kuweza kuongeza uelewa wa kutambua noti ambazo sio halali.