CHAN 2024: Guinea, Algeria ngoja tuone

FAINALI za CHAN 2024 zinaingia wiki ya pili leo Ijuma tangu zilipoanza rasmi Agosti 2 na zitapigwa mechi mbili za Kundi C, mapema saa 11:00 jioni Guinea itavaana an Algeria, huku usiku ni zamu ya Niger itakayoumana na Afrika Kusini kila timu ikisaka ushindi muhimu.

Kundi hilo linalocheza mechi zake kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, jijini Kampala Uganda hadi sasa linaoongozwa na wenyeji Uganda yenye pointi sita baada ya kushuka uwanjani mechi tatu ikifuatiwa na Algeria yenye pointi nne sawa na Afrika Kusini.

Hata hivyo, Algeria na Afrika Kusini kila moja imecheza mechi mbili, huku Guinea ikifuata nyuma yao na pointi tatu baada ya kucheza mechi tatu wakati Niger inaburuza mkia bila ya kuwa na pointi yoyote licha ya kushuka uwanjani mara mbili.

Hivyo, mechi ya leo kwa Guinea ni ya kukamilisha ratiba, tofauti na timu nyingine za kundi hilo zitakazokuwa zikikamilisha mechi za raundi ya tatu sawa na wenyeji Uganda, lakini ikihitaji ushindi ili kujiweka pazuri katika nafasi ya kuwa kati ya timu mbili za kutinga robo fainali kuifuata Tanzania.

Hii ni mechi ya 11 kwa Guinea na Algeria kukutana tangu 1980 katika mechi tofauti zikiwamo za mashindano na za kirafiki, huku rekodi zikionyesha katika mechi 10 za awali, Mbweha wa Atlas wameonekana wababe wakishinda mara tano dhidi ya nne za Guinea na zilizobaki zikiisha kwa sare.

Katika mechi ya mwisho baina ya timu hizo iliyopigwa Juni mwaka jana ya kuwania fainali za Kombe la Dunia 2026, Guinea iliitambia Algeria ikiwa nyumbani kwa mabao 2-1, hivyo pambano la leo ni la kisasi baina ya timu hizo na utamu zaidi ni kila moja imetoka kupata matokeo tofauti.

Guinea ilikumbana na aibu kutoka kwa Afrika Kusini iliyowashona mabao 2-1, siku chache tangu wafumuliwe pia mabao 3-0 na wenyeji Uganda, wakati Algeria ililazimishwa sare ya 1-1 na Wasauzi baada ya kuanza michuano na ushindi wa 3-0 dhidi ya Uganda.

Mechi ya leo ina uzito kwa timu zote kwani kuvuna pointi tatu zitaziweka pazuri, kama ilivyo kwa mchezo kati ya Niger na Afrika Kusini zitazovaana saa 2:00 usiku, ikiwa ni pambano la nne baina yao katika michuano ya CAF tangu 2010, huku Wasauzi wakiongoza kwa kushinda mara mbili katika mechi tatu zilizopita na Niger ikishinda moja zilipokutana katika mechi ya kufuzu Afcon mwaka 2011.

Katika mechi hiyo wenyeji Niger ilishinda 2-1, hivyo leo zinapokutana usiku Banyana Banyana itakuwa na kazi ya kulipa kisasi kwa wapinzani wao ambao wamepoteza mechio zote za awali kwa kufungwa na Guinea na Uganda na kuiacha ikae mkiani ikizibeba timu zote za kundi hilo.

Ushindi kwa Afrika Kusini itakayoongozwa na nahodha Neo Maema anayetajwa kusajiliwa Simba, utaifanya ikae kileleni na kuing’oa Uganda, lakini ikitegemea matokeo ya mechi ya mapema jioni, kwani Algeria yenye pointi nne pia ina nafasi ya kuwatoa wenyeji ikishinda na kufikisha pointi saba.

Timu mbili za kundi hilo zitatinga robo fainali na kucheza na washindi wa Kundi D ambao mechi zao zinapigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ambalo linalongozwa na Sudan.

Kabla ya mechi za jana ni Tanzania pekee ndio iliyokuwa imeshatinga robo fainali mapema baada ya kuongoza Kundi B ikiwa timu pekee iliyoshinda mecho zote katika fainali hizo za nane na kufikisha pointi tisa na sasa inasubiri mshindi wa pili wa Kundi A kuvaana nao Agosti 22 Uwanja wa Mkapa.