CRDB KANDA YA KUSINI YATOA WITO KWA WAKULIMA KUCHANGAMKIA MIKOPO YA RIBA NAFUU

 Na mwaandishi wetu Lindi 

BENKI ya CRDB Kanda ya Kusini imetoa wito kwa wakulima kuchangamkia mikopo ya riba nafuu,ambayo inatolewa na Benki hiyo kwa wakulima nchini ili kuwawezesha kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi kwenye sekta ya kilimo.

Meneja Mahusiano wa Benki hiyo Kanda ya Kusini,Adamu Yusufu amesema mikopo hiyo inatolewa kuptia programu ya TACATDP (Tanzania Agriculture Climate Adaptation Technology Deployment Program) ambayo ni mahsusi  ya Benki hiyo kwa ajili ya kutoa mikopo ya riba nafuu, mafunzo, bima na udhamni kwa wakulima wa mazao ya chakula ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa wakati wa kilimo, kuhifadhi mazao yao.

“Programu imelenga kutoa mikopo nafuu kwa wakulima wa chini, kati na wa juu kuwasaidia kuongeza uhimilivu wa athari za mabadiliko ya hali ya hewa wakati wa kilimo,kuvuna kuhifadhi na kuuza mazao yao,” amesema.

Adamu amesema kupitia mikopo hiyo wakulima wanawezeshwa kumudu techkonolojia,  kununua zana bora za kilimo hasa za asili zenye kulinda mazingira na kutunza rutuba ya udongo.

Amesema jumla ya dola milioni 200 zimetolewa na Benki hiyo kupitia mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kusaidia nchi kutatua changamoto za mabadiliko ya hali ya tabia ya nchi (Green Climate Fund) kwenye sekta ya Kilimo kwa mazao ya chakula huku akisisitiza wakulima kuchangamkia fursa hiyo kufanya kilimo chenye tija na kuongeza usalama wa chakula nchini.

Adamu amesema mkulima yeyote ambaye anataka kununua au kutumia mbinu bora zenye kuongeza ufanisi na mavuno shambani kwake anaweza kuomba mkopo huo.

“Kupitia programu mkulima anapata mikopo ya mtaji wa muda mfupi ambao utalipwa baada ya mavuno, mikopo ya muda wa kati na mikopo ya muda mrefu,” amesema.

Amesema kupitia programu hiyo wakulima wanapewa semina mbalimbali jinsi ya kulima kupanda na kupata mazao mengi kwa kutunza mazingira.

Program hiyo pia inatoa mikopo kwa ajili ya ununuzie wa mbegu bora kwa wakulima wote, (chini, kati na juu) ununuzi wa mbolea za asili zenye kutunza rutuba.