Dar es Salaam. Familia moja mjini Songea, mkoani Ruvuma imeingia kwenye mgogoro wa mali baada ya baba mkuu wa kaya kufariki dunia ghafla bila kuacha wosia.
Mgogoro umesababishwa na kitita cha Sh150 milioni alichokiacha benki na mali nyingine zisizohamishika, ambazo baba huyo aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa vifaa vya ujenzi ameacha.
Mzazi huyo (jina linahifadhiwa) aliyefariki dunia kwa tatizo la shinikizo la damu, aliacha mjane na watoto wanane, sita wa ndani ya ndoa na wawili wa nje.
Tangu kifo chake, familia imejikuta katika mvutano; nani anapaswa kusimamia mirathi na ni nani warithi wake. Kila upande unadai haki ya usimamizia wa mirathi.
Mmoja wa wanafamilia (jina linahifadhiwa) anasema mgogoro ulianza pale watoto wa ndani ya ndoa walipowasiliana na benki ili kufunga akaunti ya marehemu baba yao, wakieleza wao ni warithi halali.
“Benki ilikataa kutekeleza hilo bila nyaraka rasmi, waliulizwa kama kuna wosia au hati ya usimamizi wa mirathi kutoka mahakamani? havikuwepo, hapo ndipo changamoto ilianza,” anasema na kuongeza:
“Mama alikuwa na matumaini kuwa watoto wangekubaliana kwa amani, lakini hali imebadilika. Kila mmoja anamtuhumu mwenzake kuwa anataka kujinufaisha peke yake, fedha alizoacha mzee zimeleta mgawanyiko mkubwa, hakuna tena maelewano katika familia,” anasema.
Mbali ya familia hiyo, Halima Suleiman, mkazi wa Tabata, Dar es Salaam anasema amekwaa kisiki kupata urithi wa fedha zilizoachwa benki na baba yake.
Anadai kwa takribani miaka mitatu sasa anafuatilia Sh200 milioni zilizoachwa na baba yake mzazi aliyefariki dunia mwaka 2022.
“Mimi kama mtoto mkubwa wa marehemu nilijipa jukumu la kuhakikisha mali za baba zinagawanywa kwa haki,” anasema Halima, mtoto wa kwanza kati ya watano wa Suleiman.
Anadai licha ya kuwasilisha hati ya kifo, ushahidi wa uhusiano wa kifamilia na barua ya mirathi kutoka Mahakama ya Mwanzo, bado amekuwa akidaiwa nyaraka nyingine na benki.
“Nimekuwa nikipiga simu, kufika ofisini kwao mara kwa mara, hata kuandika barua rasmi, lakini kila mara kuna kisingizio kipya. Wakati mwingine wananiambia taarifa za akaunti zinahitajika kutoka makao makuu au bado wanashughulikia mchakato wa uthibitisho wa wosia,” anadai.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), Theobald Sabi akizungumza na Mwananchi amesema kuna mchakato wa kufuatwa na warithi ili kupata fedha zilizoachwa na ndugu yao aliyekuwa mteja wa benki.
Godwin Semunyu, akitoa ufafanuzi kuhusu mchakato huo kwa maelekezo kutoka kwa Sabi, amesema ili mtu arithi fedha zilizoachwa na mteja aliyefariki dunia, kwanza ni lazima awe amepitishwa na familia kama msimamizi wa mirathi.
Semunyu ambaye ni mkuu wa kitengo cha uhusiano NBC katika mahojiano na Mwananchi amesema:
“Si kuthibitishwa kwa maneno, na hii ndiyo changamoto ambayo tunakutana nayo sana, wengi wanakuja, sawa ni kweli amefiwa na ndugu yake ni mteja wa benki, lakini bila document (nyaraka) ni ngumu kusaidika.”
Amesema msimamizi anapopitishwa ataingizwa kwenye mirathi na kutambulishwa rasmi benki, kwamba ndiye msimamizi wa mirathi ya marehemu aliyekuwa ameingia mkataba na benki.
Anasema familia inapomtambulisha, hutambulisha pia akaunti ambayo fedha zilizoachwa na marehemu zitapelekwa.
Kuhusu muda wa kushughulikia mirathi hadi kupata fedha, anasema inategemea na namna familia ilivyofuata taratibu za mahakama, uwakili na familia.
“Maelekezo ya mawakili, familia na mahakama ndiyo benki huyafuata, hapa issue (suala) ni kwamba, msimamizi wa mirathi ili athibitishwe anapitia sehemu nyingi,” anasema na kuongeza:
“Mirathi siyo benki tu, kuna ardhi na mambo mengine, ile ni document (nyaraka) moja, huwa inachukua muda kwa kuwa kule kote lazima uwe signified (umetoa taarifa rasmi), baada ya hatua hizo ndipo unakuja benki pamoja na nyaraka hiyo,” anasema.
Akitoa mfano anasema, kama familia itasema marehemu alikuwa na nyumba tatu, ana akaunti kadhaa za benki, kwenye simu yake alikuwa na fedha, hayo maeneo yote lazima kipatikane kitu kimoja ambacho kinatengenezewa nyaraka moja.
“Hiyo nyaraka ndiyo inatumika sehemu zote hizo, hii ndiyo inasababisha mirathi hadi kutoka ichukue muda, ingekuwa ni maneno tu, basi wanaostahili wasingekuwa wanapata hiyo mirathi, ingekwenda kwa wasiostahili,” anasema.
Anasema katika mirathi, mahakama ndiyo hutoa amri, inaelekeza moja kwa moja fedha za mteja aliyefariki dunia zipelekwe wapi.
“Kama mteja (marehemu) alikuwa na akaunti nyingi za benki kuna judicial akaunti, lakini kwa benki sisi tunatumia court order (amri ya mahakama) ambayo nayo lazima tujiridhishe nayo kama ni ya kweli,” anasema.
Anasema benki haiwezi kuwa na notisi kama mteja wake amefariki dunia au la na haiwezi kuthibitisha hilo bila nyaraka kutoka mahakamani.
“Ikitokea mtu huyo anajulikana na kifo chake kimejulikana, kama taasisi hamuwezi kukaa kimya, mtaijulisha familia ili ifuate taratibu za kurithi,” anasema.
Changamoto kubwa inayowakabili watu anasema ni kutojua wapi au nini wafanye pale inapotokea mpendwa wao amepoteza maisha na kuacha fedha benki.
“Wengi wanakuja, anakwambia mimi ni mke wa marehemu au mtoto wa marehemu, sawa ni kweli, lakini mirathi haipo hivyo. Wosia ni muhimu kwani hata ukienda mahakamani ni kigezo kikubwa. Kuandika mirathi inasaidia hata wengine waliaochwa nje,” anasema.
Katika mirathi, anasema familia inapaswa kufahamu hairithi tu mali alizoacha marehemu, bali pia madeni aliyoyaaacha na mahakama ikiyathibitisha, warithi wanayalipa.
Semunyu anasema kwa fedha ambazo familia haina taarifa zake, kuna kipindi cha kuwa benki na kisha huhamishiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
“Baada ya miaka 10 zinahamishiwa BoT, ingawa kuna nyakati kulikuwa na mjadala wa muda wa miaka 10 upunguzwe. Hata hivyo, kama benki hatuwezi kuthibitisha mteja wetu amefariki dunia, ikitokea wakaibuka ndugu kwenye mirathi, tutawapeleka mahakamani na mahakama ndiyo itawapeleka BoT,” anasema.
Mtaalamu wa sheria, Wakili Edson Kilatu anasema kuna changamoto ambazo kwa sehemu zinachangiwa na sheria, uelewa na mtizamo wa jamii.
Kuhusu sheria anasema Tanzania haina sheria moja isipokuwa inashughulikiwa kimila, kidini (Kiislamu) na Sheria ya Serikali ya Mirathi (India Succession Act 1865).
“Sheria ya India inatumika kwa watu ambao si waumini wa Kiislamu na hawapo kwenye sheria za kimila, mtu akifariki dunia cha kwanza mnaanza kuangalia ni sheria gani inapaswa itumike,” anasema.
Kilatu anasema katika kujadiliana, wengine watadai marehemu ni kabila fulani kwa hiyo sheria za mila zinamhusu, lakini wengine wataibua alikuwa kabila fulani lakini dini yake ni fulani.
“Mvutano mara nyingi unaanzia katika eneo hilo,” anasema na kuongeza kuwa, sheria ya Kiislamu inampa mgawo mkubwa mwanamume, hivyo mwanamke anakataa kuitumia akitaka itumike sheria ya Serikali.
“Sheria ya India inasimamia na kutoa mgawanyo sawa, changamoto zinaanzia hapo na kuibuka mvutano,” anasema.
Ukiondoa sheria ya kimila na Kiislamu, anasema sheria nyingine hazina kanuni ya mgawanyo unatakiwa uweje.
“Tungekuwa na sheria moja na kanuni za utatuzi ingekuwa jambo nzuri, ingawa kuwa na sheria moja ni ngumu kwa sababu mirathi mbali ya kuwa ni sehemu ya mila pia ni ibada kwa Usilamu,” anasema.
Anasema ukitaka kutengeneza sheria nyingine, tafsiri yake utaathiri haki ya wengine kuabudu kwa kuwa mirathi ni sehemu ya ibada, ingawa changamoto nyingine ni watu kutokuacha wosia.
“Mtu akiacha wosia mzuri unasema kabisa mali zake akifa zifanyweje, kama mjane atapata kiasi fulani, ingeweza kusaidia ingawaje pia mtazamo wa kijamii na ubinafsi hata ukiacha wosia baadhi wanaweza kwenda kupinga na kubishana kwa muda mrefu mahakamani hadi ije kuamua inachukua muda,” anasema.
Kilatu anasema kinachosumbua kwenye mirathi ni tamaa ya mali kwa baadhi ya watu, licha ya kuwa kila mtu akifa inajulikana warithi wake ni kina nani.
Wataalamu wa saikolojia ya familia wanasema athari za mchakato wa mirathi huacha majeraha ya kihisia kwa wengi, hasa watoto na huathiri mfumo mzima wa familia katika vizazi vijavyo.
Wanaeleza suluhu inaweza kupatikana iwapo watu watajifunza umuhimu wa kuandika wosia mapema, kuwa wazi kuhusu mali zao na kuweka mifumo ya haki ya kugawana urithi.
Mtaalamu wa saikolojia, Modesta Kamonga amesema jamii imekuwa ikiathirika kwa sababu mtu yeyote anakuwa na ratiba na ni matamanio ziende kama alivyopanga, ikishindikana zinasababisha msongo wa mawazo.
“Msongo wa mawazo unasabisha mivutano na familia yake kwa sababu ratiba zimeenda tofauti, migogoro inakuwa mikubwa, na wakati mwingine unakuta warithi ni familia ya marehemu lakini upande mwingine unazitaka,” amesema.
Anasema watu wengi hawana utaratibu wa kuandia wosia, hivyo mtu akifariki ghafla, familia inabaki kwenye sintofahamu.