KESHO Ijumaa Azam FC inatarajiwa kuwatambulisha wachezaji wapya wawili iliyowasajili kutoka klabu ya Al-Hilal ya Sudan.
Nyota hao wanatua Azam kuungana na kocha Florent Ibenge waliyefanya naye kazi wote walipokuwa Al Hilal.
Nyota hao wapya ni, kipa Issa Fofana na mshambuliaji Taieb Ben Zitoun, ambao wameshafanyiwa vipimo vya afya na kufuzu.
Azam itawatambulisha kabla ya kuanza safari ya kwenda Rwanda kwa ajili ya kambi ya mwisho yq maandalizi ya msimu ujao wa mashindano.
Fofana aliyezaliwa Januari 30, 2004 anakuja kuziba pengo la kipa Mohamed Mustafa anayedaiwa wameachana naye kwa makubaliano baada ya msimu uliyopita kumaliza Ligi Kuu Bara akiwa na clean sheet 10.
Kwa upande wa Zitoun aliyezaliwa Tunisia mwaka 1997 ataongeza nguvu eneo la ushambuliaji akiungana na Mkongoman, Japhte Kitambala aliyetambulishwa mapema wiki hii.
Azam inaachana na Mustafa alijiunga nao Februari 7, 2024 akitokea klabu ya El Merreikh ya Sudan.
Chanzo cha ndani kilisema wachezaji hao ni pendekezo la kocha Florent Ibenge, timu wanayotokea wachezaji hao aliifundisha hivyo anaamini katika uwezo wao.
“Aliomba muda wa kuwaangalia wachezaji wote, baadaye akatwambia hataendelea na kipa Mustafa akampendekeza Fofana, tumelifanyia kazi hilo na tayari atakuwa sehemu ya timu,” kimesema chanzo hicho na kuongeza;
“Mbali na Mustafa kuna wachezaji wengine wanaweza wakaachwa, ndipo maana unaona kasajiliwa mshambuliaji Zitoun, yote hayo tunawekeza kwa sababu tunahitaji kufanya vitu vikubwa msimu ujao.”