Hatma kesi na uchaguzi TFF kujulikana leo

HATMA ya  Uchaguzi Mkuu wa  Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), uliopangwa kufanyika kesho Jumamosi, Agosti 16, 2025, itafahamika saa 10 jioni wakati Mahakama itakapotoa uamuzi wa mapingamizi ya TFF katika shauri linaloikabili pamoja na uamuzi wa maombi kusimamisha kwa muda.

‎Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Agosti 16, 2025 mjini Tanga kwa ajili ya kupata viongozi wapya akiwamo Rais na wajumbe sita wa Kamati ya Utendaji ambapo wagombea 10 wamejitokez kwa nafasi hiyo, huku Urais ukiwa na anayetetea kiti, Wallace Karia.

‎Uchaguzi huo ulionekana kuwa njia panda kufanyika, kufuatia shauri lililofunguliwa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam na mawakili wanne.

Shauri hilo la maombi namba 19873/2025, linalosikilizwa na Jaji Mfawidhi Salma Maghimbi  limefunguliwa na  mawakili wanne, Aloyce Komba, Jeremiah Mtobesya, Deusdedit Luteja na Denice Tumaini, chini ya hati ya dharura.

‎Wajibu maombi katika shauri hilo ni Baraza la Taifa la Michezo (BMT) lenye dhamana ya usimamizi wa michezo yote nchini, ambalo ndilo mjibu maombi  wa kwanza; Wadhamini wa TFF (mjibu maombi wa pili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), mjibu maombi wa tatu.

Waombaji wanadai, mchakato wa uchaguzi huo ni batili kwa kuwa unaoendeshwa chini ya Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi za TFF, ambazo ni batili, kwani zinakiuka Sheria, Katiba ya Nchi na Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Mwaka 1995.

‎Hivyo wanaiomba mahakama iridhie wafungue shauri la mapitio ya mahakama kuiomba itoe amri kuilazimisha  BMT kutekeleza wajibu wake wa kisheria katika kuisimamia TFF pamoja na mambo mengine, iielekeze TFF kufuta uchaguzi huo na kuanza upya.

‎Pia wanaomba wakati wakisubiri uamuzi wa maombi yao hayo ya kibali cha kufungua shauri hilo la mapitio mahakama hiyo iridhie kutoa amri ya kudumisha hali ilivyo kabla ya siku ya uchaguzi, kusubiri shauri lao kusikilizwa pande zote.

‎Mjibu maombi wa pili, Wadhamini wa TFF wameibua pingamizi la awali wakiiomba mahakama isilisikilize shauri hilo, badala yake ilitupilie mbali, wakidai kuwa lina kasoro za kisheria zisizorekebishika, huku wakibainisha hoja 10.

Jana Mahakama ilisikiliza ombi la waombaji kuamuru hali iendelee kuwa kama ilivyo sasa hadi maombi yao yatakaposikiliza pande zote, ombi ambalo Mahakama ikilikubali basi itaathiri kufanyika kwa uchaguzi huo kesho.

Hata hivyo, kutokana na pingamizi lililoibuliwa na mjini maombi wa pili, Mahakama haikiweza kutoa uamuzi huo jana badala yake iliuahirisha hadibleo baada ya kusikiliza na kuamua pingamizi hilo, kwa kuwa kuna  hoja zinazogusa mamlaka ya mahakama kusikiliza shauri hilo.

Hivyo Mahakama hiyo leo imesikiliza hoja nne kati ya kumi za pingamizi hilo, ambazo ndizo zitakazoamua kama Mahakama ina mamlaka kusikiliza shauri hilo au la.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Maghimbi ameahirisha shauri hilo hasi saa 10 atakapotoa uamuzi wa pingamizi hilo hasa katika hoja hizo.

Uamuzi huo ndio utakaomua uhai wa shauri hilo kuendelea au kukoma kuwepo mahakamani na pia ndio utakaotoa hatima ya uamuzi wa maombi ya waombaji ya kudumisha hali ilivyo kwa sasa (yaani uchaguzi usifanyike hadi shauri hilo litakaposikilizwa pande zote.

Kama Mahakama itakubaliana na hoja hizo nne za pingamizi au baadhi yake, kuwa haina mamlaka hayo, basi, shauri hilo litatupiliwa mbali na kila kitu litakuwa kimeishia hapo, uchaguzi huo kesho utafanyika kama ulivyopangwa.

Lakini kama haitakubaliana na hoja hizo za pingamizi hilo, ikiona kuwa hazina mashiko, basi itazitupilia mbali na hivyo itatamka kuwa inayo mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Uamuzi huo ndio utakaoingoza Mahakama kutoa uamuzi wa amri ya kudumisha hali ilivyo kwa sasa kutegemeana na jinsi itakavyoshawishika au kutokushawishika na hoja za waombaji.

Kama itashawisha na hoja hizo basi itatoa amri hiyo na hivyo uchaguzi huo haitaweza kufanyika kesho hadi itakapoamuliwa vinginevyo na Mahakama.

Hata hivyo, kama haitashawishika na hoja hizo, basi haitatoa amri hiyo na hivyo uchaguzi huo utafanyika kama ulivyopangwa huku shauri hilo nalo likiendelea mahakamani.

Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo leo, Wadhamini wa TFF wamewakilishwa na jopo la mawakili wanne, Ndurumah Majembe, Makubi Kunju, ‎Annette Kirethi na  Simon Barlow