Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said ameshindwa kupenya katika mchujo wa majina 13 ya wagombea ubunge Jimbo la Kongwa.
Hersi ameungana na wagombea wengine 11 ambao majina yao yameshindwa kupenya katika mchakato huo, huku aliyeshika nafasi ya pili kwenye kura za maoni Agosti 4, 2025, Isaya Mngurumi akipenya.
Mapema leo, Katibu wa CCM Wilaya ya Kongwa, Joyce Mkaugala amesema jina la Hersi lilikuwa miongoni mwa makada 24 waliojitokeza kugombea ubunge wa jimbo hilo.
Hata hivyo, kwenye orodha iliyotolewa baadaye, jina la Hersi halikuwemo, sawa na la Mwalimu Deus Seif, mgombea aliyeshika nafasi ya tatu kwenye kura za maoni.
Hii ni mara ya pili kwa jina la Hersi kuondolewa kwenye mchakato wa ndani ya CCM katika majimbo mawili tofauti.
Awali, Hersi aliomba katika Jimbo la Kigamboni lakini majina ya walioteuliwa yalipotangazwa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Amos Makala la kwake halikuwemo.
Mchakato wa kupata mgombea wa CCM Jimbo la Kongwa umerejewa upya kufuatia kifo cha Job Ndugai, Spika mstaafu na mbunge aliyemaliza muda wake jimboni humo, ambaye alikuwa ameongoza kwenye kura za maoni.