JICA yawanoa waandishi wa habari kuhusu miradi ya maendeleo Tanzania

Dar es Salaam. Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) limeendesha mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini, likilenga kuwajengea uelewa mpana kuhusu shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na shirika hilo hapa Tanzania.

Mafunzo hayo, yaliyofanyika mwanzoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam yakiambatana na ziara ya waandishi katika Shule za Mafunzo ya Ufundi Yombo kwa Watoto na Watu Wazima Wenye Ulemavu, moja ya miradi inayofadhiliwa na JICA.

Akifungua rasmi mafunzo hayo, Balozi wa Japan nchini Tanzania, Yuichi Mikami, alisema dhamira kuu ni kuwawezesha wanahabari kuelewa kwa undani shughuli za JICA na Ubalozi wa Japan, ili waweze kuziwasilisha kwa umma kwa usahihi.

“Ni muhimu wanahabari kufahamu kazi tunazofanya ili kuisaidia jamii kupata taarifa sahihi,” alisema Balozi Mikami.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkuu wa JICA Tanzania, Ara Hitoshi, alisema shirika hilo linaongozwa na maono ya “Kuongoza dunia kwa uaminifu na mahusiano ya watu kwa watu.”
alisema na kuongeza kuwa kuwa kwa zaidi ya miaka 60, JICA imekuwa ikishirikiana na Watanzania katika kubadilishana ujuzi na kusukuma mbele maendeleo ya pamoja.

Katika semina hiyo, waandishi waliwasilishwa mada mbili kuu ambazo ni “Ushirikiano wa kuaminiana na mafanikio: Kufanya kazi na Japani na JICA” na “Shughuli za JICA Tanzania katika Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mpango wa Wajitolea wa JICA”

Mada hizo zilitoa mwanga kuhusu historia, mafanikio na mchango wa JICA katika sekta mbalimbali nchini.

Katika hatua nyingine waandishi walitembelea Shule za Ufundi Yombo, mradi unaolenga kuwapatia watoto na watu wazima wenye ulemavu elimu ya ufundi stadi, ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi. Mradi huo ni sehemu ya miradi ya kipaumbele inayofadhiliwa na JICA kama njia ya kuimarisha ushirikiano wa maendeleo.

Aidha mwaka huu, JICA inaadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Mpango wa Wajitolea kutoka Japan (JOCV), ambao umekuwa chachu katika kujenga uhusiano wa kijamii na kiuchumi kati ya Japan na Tanzania, kupitia kubadilishana maarifa, ujuzi na uzoefu.