Kigogo FIFA kusimamia Uchaguzi Mkuu TFF, wajumbe vikao haviishi

Mjumbe wa Baraza la Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), Souleyman Waberi ataongoza ujumbe wa shirikisho hilo kushuhudia Uchaguzi Mkuu wa TFF utakaofanyika kesho Jumamosi, Agosti 16, 2025 jijini Tanga.

Waberi aliye pia  Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka la Djibouti, ameingia Tanga leo jioni akiwa na maofisa wengine kadhaa wa shirikisho hilo na lile la Afrika (CAF).

Ujumbe wa Waberi umefikia katika Hoteli ya Tanga Beach Resort ambako Uchaguzi huo mkuu wa TFF utafanyika.

Idadi kubwa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF ambao watashiriki uchaguzi huo tayari imewasili jijini Tanga na wanaonekana kuwa tayari kwa zoezi hilo.

Furaha ya wajumbe wengi ilionekana mara baada ya taarifa ya kutupiliwa mbali kwa ombi la zuio la uchaguzi huo  lililofunguliwa na mawakili wanne katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam.

Wajumbe hao walionekana kukaa na kusimama vikundi vikundi wakijadili kuendelea kwa mchakato wa uchaguzi huo huku baadhi ya wagombea na wapambe wao wakitumia fursa hiyo kuomba kura kwa wajumbe.

Usiku huu wajumbe na wageni mbalimbali wanashiriki hafla ya chakula cha jioni inayoendelea katika Hoteli itakayofanyikia uchaguzi.
Jumla ya wagombea 11 wanatarajiwa kupigiwa kura akiwa Wallace Karia anayetetea kiti cha Urais na wengine 10 wanaowania nafaai za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.