Kiungo Sudan asaka fursa chan 2024

KIUNGO wa timu ya taifa ya Sudan, Abdul Raouf amesema mashindano ya CHAN kwa upande wake ni fursa ya kuonekana na vigogo wa timu za Afrika.

Nyota huyo, kwenye mechi iliyopita dhidi ya Nigeria, alifunga mabao mawili kwenye ushindi wa 4-0, mechi iliyopigwa Uwanja wa New Amaan visiwani Zanzibar.

Raouf alisema mbali ya kuchukulia fursa binafsi, lakini kwa timu mipango yake ni kuifikisha hadi fainali na kunyakua ubingwa wa mashindano hayo.

“Lengo liko wazi ni kuisaidia Sudan kufika mbali kwenye mashindano na kuinua morali ya taifa letu, kuzingatia mshikamano wa timu, kugeuza kila shambulizi kuwa nafasi ya kufunga, na kuchangia kuimarisha nafasi ya Sudan kwenye mashindano,” alisema na kuongeza:

“Tupo hapa kushindania taji, si kushiriki tu, ili kuhakikisha Sudan inakaa kwenye mstari na kuwa miongoni mwa timu zitakazoweka historia kwenye mashindano haya.”

Sudan iko kileleni mwa msimamo wa Kundi D ikiwa na pointi nne, mechi ya kwanza ilitoa sare ya 1-1 na Congo, mechi ya pili ilishinda mabao 4-0 dhidi ya Nigeria, na Agosti 19 itamaliza mchezo wa mwisho wa kundi dhidi ya Senegal.