Kuishi bila ndoa katika mizani ya Uislamu

Dar es Salaam. Uelewa wa Kiislamu katika nafsi ya Muislamu hauwezi kuwa sahihi wala kamili mpaka apime kila jambo analokutana nalo katika maisha yake, liwe dogo au kubwa, kwa kutumia mizani ya Uislamu.

Hii ndiyo mizani ya kweli ambayo imejali sana nafsi ya mwanadamu na imeishughulikia kwa ujuzi na maarifa ya Mjuzi wa siri zake zote yaani Allah Mtukufu. Kwani nafsi hiyo ni sehemu ya uumbaji wake, naye anajua vichocheo vyake, anajua kilicho bora kwake na anajua kinachoitia madhara (nafsi hiyo).

Hivyo, ni lazima kuifuata hiyo njia kwa kutafuta yaliyo mema na kujiepusha na maovu. Allah Mtukufu anasema:“Na kwa nafsi na aliyeitengeneza, akaifunulia uovu wake na ucha Mungu wake.” (91: 7–8)

Utamaduni wa Kimagharibi umetuletea mfumo wa uhusiano kati ya mwanamume na mwanamke unaoitwa uhawara kwa maana kuishi pamoja kati ya mwanamume na mwanamke nje kabisa ya misingi na masharti ya ndoa ya Kiislamu. 

Kwa masikitiko makubwa mfumo huu wa Kihawara unaonekana kuwa si tatizo kabisa katika jamii ya Kiislamu hivi sasa, familia nyingi leo hii zimesheheni watoto waliozaliwa nje ya mfumo wa Sharia ya Kiislamu.

Katika tamaduni za Kimagharibi kuishi kihawara hakuna shida yoyote, kwani hakuna mamlaka ya familia juu ya vijana wao. Majukumu ya malezi huishia katika ngzi ya utotoni tu.

Hatufahamu mfumo wowote bora zaidi katika kuongoza uhusiano kati ya mwanamume na mwanamke, na katika kulinda haki na wajibu wao kwa njia bora zaidi, kuliko mfumo wa ndoa katika Uislamu.

Uislamu haukuangalia mwanamume na mwanamke au mkataba unaowaunganisha kwa mtazamo wa kinga ya haki tu, wala haukuzingatia uhusiano wao kama hisia za kimwili tu ambazo huanza na kuisha katika ladha ya muda mfupi.

Bali Uislamu ulipeleka uhusiano huo mbele zaidi kwenye hisia za kipekee zinazowatofautisha na viumbe wengine, na ukayainua hadi kiwango cha juu cha hisia za kiutu, ambazo si za kimwili pekee. Allah Mtukufu amesema:

“Na katika Ishara Zake ni kuwa amekuumbieni wake ….ili mpate utulivu kwao, na akaweka baina yenu mapenzi na huruma. Hakika katika hayo zimo Ishara kwa watu wanaofikiri.”(30: 21)

Hili linaonesha kuwa starehe ya kimwili siyo maana kuu ya mahusiano ya mwanadamu, kwani starehe hiyo inapatikana pia kwa viumbe wengine ambao si binadamu.

Hivyo, lazima kuwe na sifa ya kipekee ya kibinadamu inayomtofautisha na viumbe wengine. Zaidi ya hayo, binadamu anahitaji maana ya kina inayomhakikishia usalama wake wa kimaadili, inayolinda kizazi chake na kuuhifadhi utu wake.

Uhusiano wa kuishi pamoja bila ndoa (uhawara) hauna msingi wa taasisi imara kama ndoa, na washiriki wake hawana mtazamo wa muda mrefu kama walivyo wanandoa.

Zaidi ya hayo, tafiti zinaonesha kuwa watu wanaoishi pamoja bila ndoa huripotiwa kuwa na uchache wa furaha na kujitolea kidogo kwa wapenzi wao, tofauti na wanandoa. Tovuti ya “Live Science” iliripoti kuwa watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Virginia nchini Marikani walifanya utafiti kwa kutumia kipimo cha MRI kuchunguza ubongo wa wanandoa na wale wanaoishi pamoja bila ndoa.

Utafiti ulibaini kuwa baadhi ya sehemu za ubongo hupata mfadhaiko mdogo kwa wale wenye mahusiano nje ya ndoa. Mtafiti wa saikolojia Jim Coan alisema: wanandoa walionyesha kiwango kikubwa cha kujitolea kwa wenzi wao, jambo linalowapa hali ya utulivu na kujiamini zaidi.

Wafuasi wa mfumo wa “uhawara” hudai kuwa gharama za ndoa ni kubwa sana, na kwamba baadhi ya gharama hizo zinasababishwa na hali ngumu ya kiuchumi. Wengine hudai kuwa ni hali ya kijamii inayochochea mashindano ya kujifaharisha familia kupitia mahari kubwa, haya yote yana ukweli ndani yake.

 Hata hivyo, matatizo haya si kasoro ya mfumo wa ndoa, bali ni kasoro yetu sisi na mitazamo tuliyoikumbatia. Dini imeweka mipaka ya wazi kuhusu jambo hili. Mtume (rehema na amani ziwe juu yake) amesema:

“ Atakapowajia mnayeridhishwa na dini na tabia yake njema, muozesheni. Msipofanya hivyo, itazuka fitna na ufisadi mkubwa katika ardhi.”(At-Tirmidhiy)

Madai ya kuhalalisha uhawara (kuishi pamoja bila ndoa) ni dhihirisho la kupinga dini na maumbile ya mwanadamu (Al-Fitra), ni kufuta utambulisho wa kimaarifa na kiimani. Uislamu umeweka uhusiano wa mwanamume na mwanamke katika mfumo bora wa Kisharia, unaoitwa ndoa.

Mfumo huu unahifadhi heshima ya jinsia mbili hizi, unalinda jamii, na unahakikisha haki zao pamoja na haki za watoto wao. Kwa sababu hiyo, Uislamu umekataza uhusiano wa kingono nje ya ndoa. Umeharamisha pia njia zinazoelekea huko. Na umeupa jina lake halisi la zinaa.

Zinaa ni moja ya madhambi makubwa. Mwenye kuifanya huvunja mipaka ya dini, huchafua heshima ya jamii, huathiri maadili ya kijamii, na huanguka katika shimo la matamanio ya kinyama Allah Mtukufu ameita tendo hilo “fahisha” (uchafu mkubwa), na akabainisha kuwa adhabu yake ni mbaya katika dunia na Akhera. Amesema:“Wala msikaribie zinaa. Hakika hiyo ni uchafu mkubwa na njia mbaya.”(17: 32)