PAMBA Jiji imeendelea kuimarisha kikosi chake kwa kuleta wachezaji wa maana na kuachana na wale ambao haijaridhishwa na viwango vyao baada ya msimu uliomalizika kunusurika kushuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara.
Miongoni mwa nyota wapya waliosajiliwa ni timu hiyo yenye maskani yake jijini Mwanza, ni viungo wawili wazawa, Najim Mussa ambaye ni kiungo mshambuliaji kutoka Singida Black Stars aliyekuwa anacheza la mkopo Namungo.
Mwingine ni kiungo mkabaji, Kelvin Nashon kutoka Singida BS na nyota hao wawili walitambulishwa juzi Agosti 13, 2025 na klabu hiyo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Nyota hao wanaungana na wachezaji wengine saba waliosajiliwa hadi sasa, ambao ni straika Henry Lutonja (U-20), kiungo Shaphan Siwa (Kenya), kipa Arijifu Ali Amour (Azam), Hassan Kibailo (beki wa kulia).
Wengine ni nyota wa zamani wa Simba, Abdallah Hamis (mchezaji huru), beki wa kushoto kutoka Fountain Gate, Amos Kadikilo na mshambuliaji kutoka Zanzibar, Abdallah Iddi.
Wachezaji hao wapya wanapishana na wengine 10 walioachwa, ambao ni Deus Kaseke, Lazaro Mlingwa, Modou Camara, Ibrahim Isihaka, George Mpole, Cherif Ibrahim, Abalkassim Suleiman, Mwaita Gerezani, Paul Kamtewe na Ally Ramadhan ‘Oviedo’.
Akizungumzia maboresho hayo, Afisa Habari wa Pamba Jiji, Moses William alisema lengo ni kufanya vizuri msimu ujao na kuepuka changamoto zilizowakuta msimu uliopita.
Alisema benchi jipya la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Francis Baraza raia wa Kenya linaendelea na maandalizi ya msimu mpya huku likianza kutoa matumaini kwa kuboresha baadhi ya vitu kwenye timu ikiwemo kuwajengea ari ya upambananaji wachezaji.
”Tathmini ya kijumla chini ya kocha mpya viko vitu vya kiufundi ambavyo vinabadilika, eneo la uhamasishaji anafanya asilimia 100, anajua kusukuma wachezaji ili kutoa walichonacho,” alisema William na kuongeza;
“Pia anazingatia nidhamu ya muda, kuna vitu vingi sana vimebadilika, vingine vinakuja vya ndani siwezi nikavisema sana lakini kimsingi ni kocha mzuri ambaye tunaamini atatutoa tulipokuwa kwenda sehemu nyingine.”
Kuhusu watakakoweka kambi ya maandalizi ambayo msimu uliopita walikwenda Morogoro, William alisema bado uongozi unaendelea na mazungumzo kuona sehemu sahihi itakayofaa huku wakisubiri wachezaji wote waripoti kambini.
”Yako maongezi na yapo mambo ya kiuongozi yanaendelea ya kutoka na kiukweli tutatoka, ila kuhusu tunakwenda wapi na lini bado haijafahamika kama tutarudi Morogoro ama sehemu nyingine,” alisema William.