UONGOZI wa Coastal Union uko katika mazungumzo ya kumsajili aliyekuwa kiungo wa Kagera Sugar, Jofrey Manyasi, baada ya nyota huyo kuvutiwa na ofa aliyowekewa mezani, huku kilichobakia kwa sasa ni mwenyewe kusaini mkataba wa mwaka mmoja.
Nyota huyo ameondoka Kagera Sugar iliyoshuka daraja msimu wa 2024-2025, ikitoka Ligi Kuu Bara na kwenda kushiriki Ligi ya Championship msimu wa 2025-2026 NA anatafuta changamoto sehemu nyingine huku Coastal Union ikiongoza vita hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Jofrey alisema hadi sasa kumekuwa na ofa nyingi ambazo ameletewa mezani, ingawa menejimenti yake inaendelea kuzifanyika kazi kwa haraka, japo muda sio mrefu mashabiki zake watajua ni timu gani pia atakayoichezea.
“Kila kitu kinaenda vizuri na kwa sasa kuna mipango mbalimbali ambayo menejimenti yangu inaiweka sawa na itakapokamilika nitawafahamisha, suala la kubaki Kagera Sugar hilo halipo kwa sababu tayari nimemaliza mkataba wangu,” alisema Jofrey.
Kiungo huyo wa zamani aliyewika na timu mbalimbali zikiwemo Geita Gold na Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars, licha ya kauli yake ila Mwanaspoti linatambua tayari amekamilisha usajili huo, huku akipewa mkataba wa mwaka mmoja tu.
Chanzo kutoka uongozi wa Coastal Union, uliliambia Mwanaspoti Jofrey amekamilisha dili hilo kwa ajili ya kutua kikosini humo, huku mabosi wa timu hiyo wakifanya siri kubwa ya usajili, kwa sababu ya kutotaka kutibuliwa mipango yao.
Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua chanzo cha viongozi wa kikosi hicho kutotaka kufanya usajili kwa mbwembwe kama kawaida yao ni kutokana na baadhi ya nyota waliowachagua mwanzoni kutimkia kwingine, kutokana na kutokuwa na misuli ya kifedha.