Dar es Salaam. Safari ya mwanasiasa Luhaga Mpina kuwania urais kwa tiketi ya ACT Wazalendo, imeanza kuwekewa vizingiti baada ya mmoja wa makada wa chama hicho kuandika barua ya kupinga uamuzi wa mkutano mkuu maalumu uliompendekeza kuwania nafasi hiyo.
Pingamizi hilo limeandikwa na wanachama huyo, akidai uteuzi wa Mpina kuwania nafasi hiyo, umekiuka kifungu cha 16(1) (4)i cha Kanuni za Kudumu za Uendeshaji Chama toleo la mwaka 2015.
Kwa mujibu wa kifungu hicho; “Wagombea wa urais/viongozi wa chama katika ngazi ya Taifa anatakiwa awe mwanachama wa ACT-Wazalendo kwa muda usiopungua mwezi mmoja kabla ya tarehe ya mwisho ya uteuzi ya wagombea wa chama.”
Kwa mujibu wa barua ya pingamizi hilo, Mpina alijiunga na kusajiliwa kuwa mwanachama wa chama hicho, Agosti 5, 2025 na siku iliyofuata akapitishwa na mkutano mkuu kuwa mgombea wa urais, akiwa ni mwanachama wa chini ya mwezi mmoja ndani ya ACT Wazalendo.
Mwanasiasa huyo alipendekezwa kuwania urais kupitia chama hicho, Agosti 6, 2025 siku moja baada ya kujiunga na chama hicho, akitokea Chama cha Mapinduzi (CCM), alipohudumu kwa nafasi mbalimbali ikiwemo kuwa mbunge wa Kisesa kwa miaka 20.
Hatua hiyo dhidi ya Mpina, inakuja siku ambayo amechukua fomu ya uteuzi katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), jijini Dodoma na tayari ameeleza mipango yake na uamuzi wake wa kujiunga na ACT- Wazalendo.
Katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika Agosti 14, 2025, Mpina alisema atakapopewa ridhaa ya kuwa Rais atatumia jukwaa la hotuba baada ya kiapo kushughulika na wabadhirifu na kutangaza kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya.
Barua ya pingamizi, imetumwa kwa Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC.
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema kwa kuwa yuko nje ya ofisi kwa shughuli za kazi, hana taarifa hizo, ingawa anazifuatilia.
“Ngoja nizifuatilie naweza nisijue kwa sasa kwa kuwa nipo nje ya ofisi kwa shughuli za kikazi. Nipo safarini kwa masuala ya kazi. Lakini nafuatilia na nitakwambia,” amesema.
Hata Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele amesema barua haijamfikia labda Mkurugenzi wa INEC, Ramadhan Kailima ndiye anayeweza kuwa na taarifa za kina.
Mwananchi limemtafuta Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu kwa simu ambayo imeita bila kupokewa.
Alipotafutwa Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano wa ACT Wazalendo, Shangwe Ayo amesema: Sisi hatujui, hatupo ofisini tumekuja Tume (INEC), tukirudi tukaiona basi tutakufahamisha.”
Barua hiyo iliyoandikwa na Katibu Mwenezi wa ACT- Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala (nakala tunayo), inadai Mpina hajakidhi kanuni za kudumu za uendeshaji wa chama toleo la mwaka 2015.
Barua hiyo imerejea vifungu hivyo, ikieleza Mpina amejiunga chama hicho na baada ya siku mbili amepewa ridhaa ya kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho, ilhali ni kinyume na kanuni.
“Aidha, mgombea wetu amepingana na kanuni namba 16 (4) (m) inayosema “awe tayari kutangaza mali binafsi na vyanzo vyake kabla ya kuteuliwa kugombea kwa kufuata utaratatibu ulioainishwa katika sehemu ya VI ya nyongeza ya Katiba ya ACT-Wazalendo.
“Ama kwa bahati mbaya au kwa makusudi, mgombea wetu amevunja kanuni hii kwa kuwa hadi anatangazwa kuteuliwa kuwa mgombea, hakuna pahala popote ameonyesha kutangaza mali zake,” ameeleza.
Sambamba na kanuni hizo, Monalisa ambaye amekiri kuandika barua hiyo, ameeleza kuwa, mgombea huyo pia amekiuka kanuni namba 16(4)(iv) inayomuhitaji kuielewa itikadi, falsafa, misingi na sera za ACT Wazalendo na aonyeshe utayari wa kuisimamia na kuiishi”.
Amemweleza katibu mkuu kuwa, katika mabadiliko ya kanuni za uendeshaji wa chama toleo la mwaka 2024 zinazohusu chaguzi za ndani ya chama, mgombea huyo anapingana na mahitaji ya kikanuni ya sehemu ya nne 8(a) inayomtaka mgombea wa uchaguzi ndani ya chama, awe mwanachama kwa kipindi kisichopungua siku saba kabla ya mchakato wa uchaguzi kuanza.
“Kwa msingi wa uchaguzi wetu mheshimiwa Mpina, alipaswa kuwa mwanachama siku saba nyuma ya siku ya tangazo la uchaguzi lililotolewa na Katibu Mkuu tarehe 18 Aprili 2025,” imeeleza barua hiyo.
Kupitia barua hiyo, Monalisa amemtaka katibu mkuu kwa kile alichoandika kwa masilahi mapana ya chama hicho, mchakato huo uangaliwe upya ili kupatikana mgombea anayekidhi matakwa ya kikanuni, ili wasijikute wakikosa mgombea kwa mujibu wa sheria za uchaguzi ambazo mgombea wetu hakidhi.