Self microfinance kuwatoa watanzania kwenye mikopo ya kausha damu

Taasisi ya Self Microfinance Fund (Self Fund) imeeleza mikakati ya kuwafikia Watanzania wengi zaidi wenye kipato cha chini wanaojishughulisha na uzalishaji mali ili kuwawezesha kujiongezea kipato na kupunguza umaskini.

Taasisi hiyo ya serikali chini ya Wizara ya Fedha ilianzishwa mwaka 2015, imeeleza pia nia yake ya kusaidia kupunguza changamoto za mikopo inayotolewa kiholela kwenye jamii na mwisho wa siku kuwaumiza watanzania ikiwemo ile maarufu kama ‘Kausha Damu’.

Sambamba na hayo yote imejizatiti kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha Watanzania asilimia 80 wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034 ambapo imeshakopesha Sh100 milioni tangu Januari hadi sasa sekta ya nishati safi.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Agosti 15, 2025 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Santiel Yona wakati akizungumza na wahariri na wandishi wa vyombo mbalimbali vya habari katika mkutano ulioandaliwa na ofisi ya Msajili wa Hazina.

Aidha, Self Fund imetangaza mpango wa miaka mitano wa kupanua huduma zake kwa wajasiriamali wadogo kote nchini. Lengo lake ni kupunguza umaskini na kukomesha vitendo vya ukopeshaji wa kinyonyaji ambavyo vimewafikisha Watanzania kwenye madeni makubwa.

Aidha, Self Fund inalenga kuongeza mtaji wa mikopo hadi Sh300 bilioni ndani ya miaka mitano ijayo, ikifikia zaidi ya wanufaika 200,000 moja kwa moja. Taasisi pia inapanga kuongeza idadi ya matawi yake kutoka 12 hadi 22 ili kufikia huduma nchi nzima.