Serikali yajizatiti kuwaokoa Watanzania na ‘kausha damu’, nishati safi

Dar es Salaam. Taasisi hiyo ya Serikali chini ya Wizara ya Fedha ilianzishwa mwaka 2015, imeeleza pia nia yake ya kusaidia kupunguza changamoto za mikopo inayotolewa kiholela kwenye jamii na mwisho wa siku kuwaumiza Watanzania ikiwemo ile maarufu kama ‘Kausha Damu’.

Sambamba na hayo yote imejizatiti kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha Watanzania asilimia 80 wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034 ambapo imeshakopesha Sh100 milioni tangu Januari hadi sasa sekta ya nishati safi.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Agosti 15, 2025 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Santiel Yona wakati akizungumza na wahariri na wandishi wa vyombo mbalimbali vya habari katika mkutano ulioandaliwa na ofisi ya Msajili wa Hazina.

“Kama taasisi ya Serikali tuna jukumu la kusaidia kupunguza umaskini na tumejikita kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo kwa masharti nafuu. Kwa kufanya hivi tunajitahidi kuwafanya wananchi waondokane na mikopo umiza kama (Kausha damu),” amesema.

Aidha, Self Fund imetangaza mpango wa miaka mitano wa kupanua huduma zake kwa wajasiriamali wadogo kote nchini. Lengo lake ni kupunguza umaskini na kukomesha vitendo vya ukopeshaji wa kinyonyaji ambavyo vimewafikisha Watanzania kwenye madeni makubwa.

“Tunajitahidi kuhakikisha wananchi wanaepuka mikopo ya mateso kama Kausha Damu.” amesema.

Aidha, Self Fund inalenga kuongeza mtaji wa mikopo hadi Sh300 bilioni ndani ya miaka mitano ijayo, ikifikia zaidi ya wanufaika 200,000 moja kwa moja. Taasisi pia inapanga kuongeza idadi ya matawi yake kutoka 12 hadi 22 ili kufikia huduma nchi nzima.

“Dira yetu ni kuongeza upatikanaji wa huduma na kuendelea kutoa elimu ya fedha sambamba na mikopo. Tunataka kila mjasiriamali wa Kitanzania iwe ni wa kilimo, biashara ya rejareja au nishati jadidifu ajue kuwa kuna chanzo salama, kilichosajiliwa na chenye gharama nafuu cha kupata fedha.”

Ameeleza katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 mpaka kufikia Juni 30, 2025 mfuko huo umetoa mikopo yenye thamani ya Sh196.9 bilioni na kiwango cha mikopo chechefu kikiwa chini ya asilimia 10.

Nchini kote, ukosefu wa elimu ya fedha umewafanya wananchi wengi kuwa wepesi wa kukopa kutoka kwa wakopeshaji wasio rasmi au vikundi visivyo na usimamizi wa kisheria.

Kiwango cha riba kwenye mikopo hiyo kisicho rasmi kinaweza kufikia viwango vya unyonyaji, masharti ya marejesho mara nyingi hayako wazi, na kushindwa kulipa kunaweza kusababisha fedheha kijamii au kupoteza mali.

“Kwa riba ya asilimia 15 hadi 22 kwa mwaka, tumeweza kuwafikia wanufaika wapatao 183,381 kati yao wanawake ni 97,170 sawa na asilimia 53 na wanaume 86,211 sawa na asilimia 47,” amesema kiongozi huyo.

Katika kusaidia kupunguza mikopo inayoumiza katika jamii, Yona amesema moja ya jukumu lingine la taasisi ni kutoa elimu kwa taasisi ndogo za huduma ya fedha.

Amesema tangu mwaka 2021 hadi Juni 2025, mfuko umezikopesha na kuzijengea uwezo taasisi 549 za huduma ndogo za fedha, ili kuzisaidia kupunguza changamoto za uendeshaji wake.

Mkurugenzi wa maendeleo ya biashara na masoko kutoka Mfuko wa Self, Petro Mataba ameeleza kuwa tayari wameanza jitihada za kupunguza matumizi ya mkaa na nishati nyingine chafu katika kupikia kwa kuwakopesha watu kwa ajili ya kutumia nishati safi.

“Kutokana na nishati safi ya kupikia kuwa moja ya kipaumbele cha Serikali, mfuko umeanza kutoa mikopo kwa ajili ya upatikanaji wa nishati safi ya kupikia. Tumetoa zaidi ya Sh100 milioni kwa wanufaika wa nishati safi zaidi ya 100 na bado tunaendelea kuhamasisha,” amesema Mataba.

Kwa kuendana na vipaumbele vya serikali, taasisi hiyo pia imeanza kufadhili miradi ya kuendeleza teknolojia za upishi safi sekta muhimu katika kupunguza ukataji miti, kuboresha afya ya umma na kupunguza gharama za nishati majumbani.

Mikopo hiyo inawawezesha wajasiriamali kununua na kusambaza majiko bora, mifumo ya biogas na suluhu nyingine za nishati safi.

“Upishi safi ni kipaumbele cha Serikali kwa sababu unapunguza utegemezi wa mkaa na kuni, ambavyo vyote ni ghali kwa familia na vina madhara kwa mazingira,” ameleza Mataba.

Moja ya changamoto ilioelezwa na wataalamu hao ni pamoja na kuwepo kwa changamoto kubwa za wananchi wengi kutokuwa na elimu ya kutosha ya kuhusu fedha. Hii imewafanya wananchi wengi kukosa uelewa wa kutosha wakati wa kufanya maamuzi ya kukopa.

“Hili ni tatizo kubwa ambalo huleta matatizo mitaani kutokana na wengine kutokuwa na utamaduni wa kurejesha mikopo yao. Hili sisi kupitia mfuko tunaendelea kulifanyia kazi kwa kutoa elimu ya kutosha kwa wakopaji,” ameeleza Yona.

Wataalamu wanasema kadri sekta ya wajasiriamali wadogo na wa kati inavyokua, ni muhimu kwa wajasiriamali kuwa makini kuhusu wanakopeshwa fedha. BoT ina orodha ya umma ya taasisi za kifedha zilizosajiliwa ambayo wakopaji wanaweza kuikagua kabla ya kukopa.

Kukopa kupitia njia rasmi kunamlinda nimkopaji dhidi ya vitendo vya kinyonyaji na pia kunaimarisha mfumo wa kifedha wa nchi kwa ujumla.