JANA jioni Simba ilimtambulisha rasmi beki raia wa Guinea, Naby Camara, lakini mapema mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Jonathan Sowah ametoa msimamo mzito, huku akimtaja kocha Fadlu Davids.
Sowah aliyesajiliwa na Simba hivi karibuni akitokea Singida Black Stars aliyoitumikia kuanzia Januari mwaka huu aliposajiliwa kupitia dirisha dogo ambapo katika mechi 15 za mashindano yote aliifungia timu hiyo mabao 14, yakiwamo 13 ya Ligi Kuu na moja la Kombe la Shirikisho (FA).
Nyota huyo raia wa Ghana juzi alifunga moja ya mabao mawili yaliyoiwezesha Simba kupata ushindi katika mechi ya kirafiki dhidi ya Kahraba Ismalia ya Misri ikitumika kama sehemu ya kambi y mazoezi ya Wekundu hao waliyoiweka jijini Ismailia. Bao jingine katika mechi hiyo lilifungwa na Mohammed Bajaber. Nyota hao wawili waliosajiliwa na kutambulishwa hivi karibuni.
Straika huyo Mghana aliyetua Msimbazi kutoka Singida Black Stars ametamba kuwa ataanzia pale alipoishia na wote waliokuwa wakimjadili vibaya, majibu yao yatakuwa uwanjani kupitia miguu kwa vile hajazoea kuongea, huku akimtaka kocha Fadlu Davids anayemnoa kikosini.
Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Misri, Sowah alisema tayari ameshaanza kuzoea maisha ndani ya familia ya Simba, ambapo sasa anasubiri jambo moja tu muunganiko wa kikosi chao.
Sowah alisema ana hesabu kubwa ndani ya kikosi hicho akitaka kuweka rekodi kubwa ya kufunga mabao kutokana na ubora wa timu, kuanzia benchi la ufundi mpaka wachezaji wenzake.
Alisema, baada ya mechi ya kirafiki ya kwanza akiwa na uzi wa timu hiyo na hata mazoezini, amekubali ubora wa wachezaji wenzake akisema uwepo wa viungo bora na hata mabeki wazuri kutampa nafasi ya kufanya vyema mara wakishapata muunganiko.
“Tunaendelea na maandalizi, tulicheza mchezo wa kwanza ndio lakini matokeo sio kitu muhimu, jambo zuri ni kwamba tunaendelea kuimarika kama timu, tukishapata muunganiko tutakuwa hatari zaidi na watu wasubiri majibu zaidi msimu ukianza kupitia miguu yangu uwanjani,” alisema Sowah na kuongeza;
“Nafurahi niliingia na kufunga, kwangu mimi ni kitu ambacho hakinifanyi nijishangae kwa kuwa ni kazi yangu, kitu muhimu zaidi ni kuona tuna timu nzuri, hapa kuna viungo bora na hata mabeki wenye viwango.
Msimu uliopita Sowah alimaliza na mabao 13 kuputia mechi 14 baada ya kusajiliwa dirisha dogo, mbali na kufunga pia bao katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Simba.
Pia Sowah amesema anavutiwa na mafunzo ya Fadlu, akisisitiza Simba itafanya makubwa kwa kuwa mbinu za kocha huyo Msauzi katika kutafuta ushindi zaidi.
“Kila mchezaji anajituma sana ili kutafuta imani kwa makocha, hicho pia nakifanya kwanza nataka kujipanga nipate nafasi ya kucheza na baada ya hapo nataka kufunga zaidi hapa kuliko nilichofanya kabla nikiwa na timu yangu iliyopita.
“Simba ni timu kubwa inataka matokeo, unaona hata kocha falsafa zake zinataka kutafuta ushindi muda wote, hili ni jambo zuri linaifanya timu kutakiwa kucheza muda wote kwahiyo kila kitu kipo sawa.”
Katika hatua nyinginer kiungo Mohammed Bajaber amefunguka kuhusu mipango aliyonayo kwa timu hiyuo na kuchimba mkwara ana matarajio makubwa ya kufanya akiwa na kikosi hicho.
Bajaber amekuwa gumzo kwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi kutokana na kiwango chake msimu uliopita akiwa na Polisi FC ya Kenya, ambapo alifunga mabao 11 na kutoa asisti nne.
“Nimepokelewa vizuri sana. Wachezaji wenzangu na benchi la ufundi wamenifanya nijisikie kama niko nyumbani. Hapa ni sehemu sahihi ya kuonyesha uwezo wangu, na ninaamini huu ni mwanzo wa safari ndefu ya mafanikio,” alisema Bajaber na kuongeza; “Siku zote mashabiki wanataka matokeo, wanataka ubora wa mchezo na burudani. Niko tayari kupigana kwa ajili yao na klabu hii. Ninachotamani zaidi ni kushinda mataji nikiwa na Simba.”
Kwa upande wa kocha Fadlu ameonyesha dhamira ya kumtumia Bajaber kama sehemu ya mpango wa mashambulizi ya kasi na kufungua ngome za wapinzani kazi ambayo ilifanywa vizuri msimu uliopita na Ellie Mpanzu na Kibu Denis katika maeneo ya pembeni.
Mbali na kuwa na uwezo wa kufunga, Bajaber anatajwa kuwa na akili kubwa ya mpira kwa kutafuta nafasi na kufanya maamuzi sahihi.
Anaweza kucheza kama kiungo mshambuliaji au winga, jambo linalompa kocha chaguo zaidi la kimbinu.
“Nafurahia mwenendo wake pamoja na wachezaji wengine wapya, bado tunakazi ya kufanya katika kipindi kilichosalia, nadhani tutaendelea kucheza michezo zaidi ya kirafiki kwa lengo la kujipima,” alisema Fadlu.
Baada ya maandalizi ya msimu ujao kukamilika huko Misri kikosi cha Simba kinatarajiwa kurejea nchini mwishoni mwa mwezi huu kwa ajili ya tamasha la Simba Day ambalo kwa mujibu wa ratiba linatarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi ujao kisha kucheza mechi za Ngao ya Jamii.