SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa elimu kwa Mawakili wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, leo tarehe 14 Agosti, 2025 kwa lengo la kujenga uelewa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu TASAC ikiwemo majukumu ya Kisheria na Mikataba ya Kimataifa, Ulinzi, Usalama na Utunzaji wa Mazingira ya Usafiri kwa njia ya maji na biashara za meli.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Wakili Judith Kakongwe amewaasa mawakili kutumia nafasi hiyo kuelewa kwa kina masuala mbalimbali ya kisheria yanayohusu uanzishwaji wa TASAC.
“Tunatamani kusikia maswali mengi au ufafanuzi mtakaouhitaji kutoka kwetu ili tuhakikishe kwamba mnaijua TASAC kwa undani na kuwarahisishia pindi mnapotoa ushauri wa kisheria ama kutoa maamuzi ya kisheria kuhusu TASAC,” amesema Wakili Kakongwe.
Wakili Kakongwe ameongeza kuwa TASAC inashirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu katika mambo mengi sana hivyo mafunzo hayo ni fursa adhimu ambayo TASAC imekuwa ikisubiri kwa muda mrefu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uratibu na Ushauri wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Bw. Ladislaus Komanya amesema lengo la Ofisi hiyo ni kuifahamu TASAC kwa kuwa taasisi hizo mbili zinashirikiana katika masuala ya upekuzi wa mikataba na ushauri wa masuala ya kisheria.
“Wataalam wetu waliopo hapa ndio wabobezi na sio kwamba tunafahamu kila kitu hivyo tukipata kazi zenu huwa tunafanya tafiti kabla ya kutoa ushauri lakini fursa hii inatupa nafasi ya kuwafahamu vizuri na kufanya kazi zenu kwa ufanisi”, amesema Bw. Komanya.
Mafunzo hayo ya siku mbili yamelenga kuwajengea uwezo Mawakili kutoka Idara ya Mikataba na Idara ya Uratibu wa Ushauri Huduma za Kisheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.