Dar es Salaam. Ni dhana iliyojengeka miongoni mwa wanajamii kwamba, jicho likicheza ni ishara ya kutokea jambo liwe baya au zuri.
Kila mmoja na mtazamo wake, wapo wanaoamini kucheza kwa jicho ama la kulia au koshoto huashiria kutokea tukio la furaha au huzuni.
Baraka John, mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam anasema siku jicho lake la kushoto likicheza huishi kwa wasiwasi akiamini ni ishara ya kupokea taarifa mbaya.
“Katika ukuaji wangu wote nimekuwa nikisikia wazazi wangu wakisema kucheza kwa jicho la kushoto ni ishara ya kupokea taarifa mbaya na mimi nimekuwa nikiamini hilo,” anasema.
Kwa upande wake, Amina Simbamwene, mkazi wa Mbagala anasema kumekuwa na dhana nyingi kuhusu kucheza kwa jicho ambazo zinaweza kutokea au zisitokee.
“Ni imani tu ambayo imejengeka kwa baadhi ya watu katika jamii,” anasema.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, hakuna ushahidi wa kisayansi au kitabibu unaoonyesha uhusiano kati ya kucheza kwa jicho na ishara ya kutokea kwa matukio mbalimbali katika maisha.
Tovuti ya afya ya Cleveland Clinic inaeleza kwa baadhi ya watu, hali hiyo huweza kujitokeza kama ishara ya kuonyesha mhusika ana uchovu, hajapata muda wa kutosha kupumzika au kuwa na msongo wa mawazo.
Akifafanua kuhusu hali hiyo alipotafutwa na Mwananchi, Daktari wa Macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe, Dk Otilia Ngui anasema kitaalamu hali hiyo hujulikana kama ‘eye twitching’.
Dk Ngui anasema hali hiyo inasababishwa na misuli midogo ya kope kukaza na kulegea kwa haraka bila hiari ya mtu.
Anasema siyo kwenye jicho pekee hata katika sehemu yoyote ya mwili wa binadamu yenye misuli hali hiyo huweza kujitokeza.
“Ni hali ya kawaida isiyo na athari ambayo mara nyingi hutokea bila ya kuwa na sababu maalumu na kwa kawaida hudumu kwa muda mfupi na kutoweka,” anasema.
Anasema kuwa wakati inaweza kutokea kwa baadhi ya watu kutokana na mtu kutopata muda wa kutosha wa kulala, uchovu au msongo wa mawazo.
Hata hivyo, mtaalamu wa lishe Dk Daudi Gambo anasema jicho na hata sehemu nyingine ya mwili inapocheza inaweza kuashiria kupungua kwa virutubisho vya aina fulani ndani ya mwili.
“Inawezekana virutubisho mfano madini yanayotakiwa katika eneo husika ili kufanya kazi vizuri yamepungua au kuzidi,” anasema.
Dk Ngui anasisitiza pamoja na hali hiyo kutajwa kutokuwa na athari, inashauriwa mhusika kumuona daktari wa macho kama hali ya kucheza kwa jicho itaongezeka kasi na itadumu kwa muda wa zaidi ya siku moja.
“Jicho likiendelea kucheza kwa kasi na kwa muda mrefu bila kutulia ni muhimu mhusika kufika hospitali na kuonana na daktari wa macho kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi,” anasema.
Dk Ngui anasema dalili nyingine ambazo mtu akizihisi katika macho yake ni muhimu kuonana na mtaalamu wa macho ni kupungua kwa uwezo wa kuona, ambao huweza kuanza kuonyesha dalili kidogo kidogo.
Pia, kuwasha kwa macho, kutokwa machozi na wakati mwingine tongotongo mara kwa mara bila sababu maalumu kwa muda mrefu.
“Maumivu makali ya macho na kichwa, macho kuwa mekundu kwa muda mrefu, kunapotokea michubuko, jeraha au uvimbe usio wa kawaida na hali nyinginezo zisizo za kawaida kwenye jicho ni muhimu kufika hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa kina,” anasema.
Daktari wa binadamu, Shitta Samweli anashauri ili kuwa na afya bora ya macho ni muhimu kuzingatia usafi wake na ulaji wa vyakula vinavyosaidia kuboresha afya ya macho.
Dk Shitta anabainisha baadhi ya vyakula hivyo kuwa ni viazi vitamu, karoti, mboga za majani, machungwa, karanga, samaki, dagaa na vinginevyo vyenye vitamini A, C na E.
Anasisitiza unywaji wa maji ya kutosha, kufanya mazoezi na kupata muda wa kutosha kupumzika.
Kwa mujibu wa tovuti ya afya ya Web MD ili kuwa na macho yenye afya ni muhimu kuepuka unywaji wa pombe kupindukia, uvutaji wa sigara na vyakula vyenye kiasi kikubwa cha sukari.
Pia, kuepuka kutazama mwanga wa jua moja kwa moja, kusoma au kutumia simu gizani, kwani mwanga hafifu hufanya macho yawe na presha zaidi na yanaweza kuchoka haraka.
“Vilevile ni muhimu kufanya uchunguzi wa macho yako walau mara mbili hadi tatu kwa mwaka hata kama hauhisi dalili yoyote hatarishi,” anasema.