Si mbio tu, mwaka huu kuna kutembea peku msituni! Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wamezindua msimu wa tatu wa Tukacharu Rau Forest Charity Tour 2025 unaokuja kwa staili mpya inayochanganya utalii, michezo na kutoa msaada kwa wenye uhitaji.
Tamasha hilo litafanyika Agosti 24, 2025 kwenye msitu wa Rau, Moshi, likihusisha mbio fupi (km 5 na 10), mbio za baiskeli na utalii wa asili wa “kutembea peku” kwa wanamichezo na wageni.
Zaidi ya watalii 10,000 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kushuhudia vivutio vya kipekee kama panya wenye masikio kama ya tembo na mvule mkubwa zaidi Afrika.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Geofrey Mnzava, amesema hamasa hii imepata nguvu kutokana na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Royal Tour, jambo lililoongeza idadi ya watalii na mchango wa sekta ya utalii katika pato la taifa.
“Mwaka huu tumekuja tofauti. Pamoja na michezo na utalii, tunagusa jamii kwa kugawa sehemu ya mapato kwa watoto wenye mahitaji maalumu, wazee na wanaolelewa kwenye makazi salama,” amesema Mnzava.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa TFS Moshi, Godson Ulomi, amesema msimu wa kwanza wa Tukacharu ulikuwa na washiriki 360 pekee, lakini mwaka jana baada ya msimu wa pili idadi ya watalii wa Rau ilipaa kutoka 6,500 hadi 11,800.
“Sasa tunarudisha shukrani kwa jamii, tukigusa maisha ya vijana 170 wenye mahitaji maalumu na makundi mengine yenye uhitaji,” amesema Ulomi.
Mratibu wa Tukio hilo, Rosemary Didas, amesema usajili ni Sh25,000 (ikiwa na kingilio cha msitu na mchango wa misaada), huku wale watakaokuja kutalii na kushiriki michezo pekee wakitozwa Sh 3,000.
“Tutawapeleka msituni, tutakula nao, tutawapa vifaa vya shule, tiba na vyakula ili wajue bado wanathaminiwa,” amesema.
Baadhi ya mashabiki wa michezo na utalii, wamesema hii ndio nafasi ya kukimbia, kuendesha baiskeli na kutembea peku msituni huku ukibadilisha maisha ya mtu mwingine.
Awali, baadhi ya wawakilishi wa makundi yenye uhitaji walishukuru TFS kwa wazo hilo la kuwasaidia na kuomba mpango huo uwe endelevu ili vituo vyao na walengwa wengine waendelee kunufaika.