Vijana wapewa mbinu kupambana na ukosefu wa ajira

Bunda. Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa,  Ismail Ussi amewataka vijana kujitokeza na kutumia fursa ya mikopo isiyokuwa na riba inayotolewa na halmashauri ili kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana nchini.

Ussi ametoa wito huo leo Ijumaa Agosti 15, 2025 mjini Bunda baada ya kukagua na kuzindua mradi wa Umoja wa Vijana Waendesha Pikipiki za usafirishaji ambapo amesema mikopo hiyo inayotokana ba mapato ya ndani ya halmashauri ikitumika vema itaondoa  kabisa suala la ukosefu wa ajirabkwa vijana.

Amesema vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ni makundi ambayo yamekuwa yakipata changamoto za kiuchumi kutokana kukosekana kwa nafasi za ajira za kutosha.

“Serikali baada ya kuona changamoto hii imekuja na wazo hili la mikopo kwa makundi haya, fursa hii ni muhimu sana kwa vijana na ikitumika vizuri kama ambavyo Serikali imekusudia basi italeta mapinduzi makubwa sana ya kiuchumi miongoni mwa vijana na katika jamii kwa ujumla,” amesema.

Amesema vijana wanatakiwa kuchangamkia fursa ya mikopo hiyo kwa maelezo kuwa pesa kwaajili ya mikopo ipo ya kutosha hivyo kila kijana mwenye uhitaji anapaswa kufuata utaratibu ikiwepo ya kuunda vikundi na kuvisajili halmashauri kabka ya kuendelea na michakato mingine.

Amewataka vijana kuwa wabunifu katika kuandaa miradi kulingana na uhitaji wa maeneo yao ili kupanua wigo wa ajira na kipato kwa vijana na jamii kwa ujumla na kwamba hakuna kikwazo kwa vijana kujikwamua kiuchumi kupitia mikopo hiyo.

Akitoa taarifa ya kikundi hicho, Katibu wa kikundi, James Thomas amesema kikundi hicho chenye wanachama watano kilipokea mkopo wenye thamani ya zaidi ya Sh12 milioni kutoka halmashauri ya Mji wa Bunda.

Thomas amesema pesa hizo walizitumia kununua pikipiki nne ambazo wanazitumia kwaajili ya usafirishaji.

Amesema awali kabla ya kununua pikipiki hizo walikuwa wakiendesha pikipiki za watu kwa mikataba maalum ambapo walikuwa wanatkiwa kuwasilisha pesa kwa wamiliki wa pikipiki kila siku bila kujali hali ya biashara kwa siku husika.

“Tulianza tukiwa na mtaji wa Sh80,000 na tulikuwa tunatakiwa kuwasilisha pesa kwa wenye pikipiki lakini sasa hivi tunamiliki pikipiki zetu zilizotokna na mkopo wa asilimia kumi tayari kipato chetu kimeanza kuimarika,” amesema Thomas.

Awali, akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Kusaya, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, Salum Mtelela amesema ukiwa katika halmashauri ya Mji wa Bunda mwenge huo unatarajia kukagua, kutembelea na kuzindua miradi minane yenye thamani ya zaidi ya Sh3 bilioni.