KWA mujibu wa taarifa kutoka Zambia vipigo vitatu mfululizo kwenye mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN 2024 yanayoendelea ukanda wa Afrika Mashariki vimemuweka kwenye wakati mgumu kocha mkuu wa Chipolopolo, Avram Grant.
Zambia, iyopo kundi A, imeondolewa rasmi kwenye mashindano hayo baada ya Alhamisi kupoteza mechi ya tatu mfululizo kwa kuchapwa mabao 3-1 na Morocco. Hiyo ilikuwa mechi iliyotarajiwa kuamua hatma yao.
Awali Chipolopolo walifungua kampeni kwa kufungwa mabao 2-0 na DR Congo katika mechi ambayo ilionekana kushindwa kabisa kumudu kasi ya wapinzani wao. Baada ya hapo, walijikuta tena wakipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Angola, licha ya kupata nafasi kadhaa za wazi ambazo walishindwa kuzitumia.
Matokeo hayo yamefanya Zambia kubaki mkiani mwa msimamo wa kundi hilo bila pointi, huku ikibaki na mechi moja ya kukamilisha ratiba. Mechi hiyo itapigwa Jumapili dhidi ya vinara Kenya, ambao wanahitaji pointi ili kumaliza kileleni na kujiweka vizuri kwa hatua ya mtoano.
Kocha Grant ambaye aliwahi kuiongoza Ghana hadi fainali ya AFCON mwaka 2015, sasa anakabiliwa na presha kubwa kutoka kwa mashabiki na wadau wa soka nchini Zambia. Wengi wanasema kuwa kikosi chake kimekosa mwendelezo na mbinu za ushindi, licha ya kuwa na wachezaji wenye uzoefu.
Kushindwa kwa Zambia katika CHAN pia kumefufua mjadala kuhusu maandalizi duni ya timu hiyo kabla ya mashindano. Wachambuzi wa soka nchini humo wamedai kuwa muda wa maandalizi ulikuwa mdogo, na hakukuwa na mechi za kirafiki za kutosha kupima uwezo wa kikosi.
Mbali na hilo, kumekuwa na malalamiko juu ya uteuzi wa kikosi, baadhi ya mashabiki wakisema majina yaliyopangwa hayakuwiana na wachezaji waliokuwa na kiwango bora kwenye ligi ya ndani. Hali hiyo imechochea mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, wengi wakimtaka Grant kujiuzulu.