Vitendo vya ufisadi, rushwa vyatajwa kudidimiza nchi za Afrika

Arusha. Vitendo vya ufisadi na rushwa na matumizi mabaya ya rasilimali za umma katika nchi nyingi za Bara la Afrika, vinatajwa kudidimiza maendeleo katika bara hilo.

Kutokana na sababu hiyo Taifa linapaswa kujenga tabia na utamaduni wa kukataa rushwa na vitendo hivyo ikiwemo kuwaibua viongozi vijana watakaolinda rasilimali.

Hayo yamesemwa jana Alhamisi Agosti 14, 2025 jijini Arusha na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza katika jukwaa la uwajibikaji kwa vijana (YAIF), kutoka Vyuo vikuu na kati nchini.

Amesema tatizo la matumizi mabaya ya rasilimali za umma ni tatizo la dunia nzima lakini katika nchi zinazoendelea zina wajibu wa kuwa makini ili vitendo vya rushwa na ufisadi visididimize bara hilo.

“Ni suala wakati mwingine linaweza kuvurugwa na mifumo hivyo kusipokuwa na mipaka,kuangalia na kupiga kelele tunaweza tukajikuta bara letu hili linaweza likarudi nyuma mno.Tufanye watu wafuatilie,wahoji lazima tujenge kama ni utamaduni na unaanza hapo ulipo usitarajie uanzie kwingine,” amesema.

“Tukitaka tuibue viongozi watakaolinda rasilimali lazima tujenge tabia kwa wetu wetu hasa vijana kwani tusipojenga utamaduni wa kuchukia ubadhirifu, ufisadi na rushwa.Kwa  kujenga tabia na utamaduni wa kukataa rushwa na ufisadi ni hatua muhimu sana kuhakikisha kwamba tunalinda na tunaweza kuziendeleza rasilimali zetu,” amesema.

 Profesa Mkenda amesema ndiyo maana somo la Historia ya Tanzania na maadili linafundishwa mashuleni kwa lengo la kuwa wazalendo ili kulinda nchi na rasilimali zake.

“Nawasihi vijana ambao ndiyo viongozi wa kesho,tuwe na uwajibikaji katika kila mnalofanya kulinda na kusimamia matumizi mazuri ya rasilimali zetu.

“Vijana ndiyo wenye nguvu kama vijana tukumbushe tulinde uwajibikaji na kuwajibika na tutumie vipaji na uwezo ulionao kuendeleza nchi yetu,”amesema.

Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh amesema klabu za vijana kutoka vyuo vikuu 11 hapa nchini, zimelenga kuongeza uelewa mpana wa uwajibikkaji na utawala bora ikiwemo kuelewa madhara ya rushwa na mapambano dhidi yake kabla ya kuingia kwenye soko la ajira au kujiajiri.

Uttoh ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Uwajibikaji kwa umma ( Wajibu),amesema jukwaa hilo lilianzishwa kwa madhumuni ya kuwaandaa vijana kuwaa viongozi bora wenye uadilifu,uadilifu,uwajibikaji na uzalendo kupitia mafunzo mbalimbali.

Amesema jukumu la uwajibikaji wa umma katika rasilimali za umma ni la kila mmoja na Taifa linategemea mchango wa vijana katika hilo hasa kufuatia ongezeko la vijana nchini.

Ametaja vyuo hivyo ni pamoja na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA),Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) ambapo washiriki ni pamoja na walezi wa mabaraza hayo ya vijana,viongozi wa vilabu vya uwajibikaji ngazi za vyuo na wajumbe wa vilabu hivyo.

“Jukwaa hili hukutana mara moja kwa mwaka ambapo pamoja na masuala mengine wanajadili na kupanga mipango ya mwaka unaofuata,kuwajengea vijana dhana ya uwajibikaji,uzalendo na mapambano dhidi ya rushwa,”amesema.

Awali akisoma risala ya jukwaa la YAIF,Magreth Clement,amesema jukwaa hilo limeandaliwa na Wajibu kwa lengo la kukuza na kuimarisha mazingira ya uwajibikaji wa fedha za umma na utawala bora nchini Tanzania.

“Wajibu imewawezesha wananchi hasa vijana kushiriki kikamilifu katika kufuatilia ukusanyaji wa mapato na matumizi ya rasilimali za umma na imekuwa mshirika muhimu katika kukuza uwazi,uwajibikaji na ushiriki wa wananchi,” amesema

Amesema jukwaa hilo lina malengo manne ambayo ni kuimarisha ushiriki wa wananchi,kuongeza uwezo wa wadau,kushawishi mabadiliko ya sera na kuimarisha  uwezo wa kitaasisi ambapo imeanzisha programu kwa vijana katika Vyuo Vikuu ikiwemo mijadala katika uwajibikaji katika taasisi za elimu ya juu.

Amesema kwa mwaka 2024/2025 wameweza kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo na taasisi na klabu za kupambana na rushwa na kushirikiana na viongozi wa serikali za wanafunzi kuimarisha uwazi wa mapato na matumizi ya fedha za serikali za wanafunzi.

Magreth ametaja changamoto wanazokabiliana nazo ni pamoja na klabu za uwajibikaji bado hazina utambulisho rasmi wa kitaifa katika shule za msingi na sekondari wakati shule hizo zinahitaji utambulisho huo ili kuwapa ruhusa ya kufanya midahalo,majadiliano na mafunzo katika shule husika.

“Pia bado hatujapata ridhaa rasmi katika baadhi ya vyuo kufuatilia mapato na matumizi ya fedha za wanafunzi katika serikali za wanafunzi na kuzidai ziweke uwazi wa mapato na matumizi ya fedha hizo,” amesema.

Mwakilishi wa walezi wa klabu ya wanafunzi kutoka Vyuo 11 vya elimu ya juu nchini, Alphonce Kauki amesema walezi wameendelea kutumia nguvu na taaluma katika kuwalea vijana kwa kuzingatia kanuni, sheria na miongozo.