WAANDISHI wa habari mkoani Dar es Salaam wamejengewa uwezo kuhusu namna ya kuripoti Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa kuzingatia usalama wao, usawa wa kijinsia, na sheria mpya za uchaguzi zilizopitishwa mwaka 2024.
Mafunzo hayo ya siku moja, yaliyoandaliwa na Kampuni ya Media Brains kwa udhamini wa Shirika la Konrad Adenauer Stiftung (KAS) kutoka Ujerumani, yalilenga kuwapa wanahabari mbinu sahihi za kutekeleza majukumu yao bila kuvunja sheria na kuepuka upendeleo wa kihabari.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Media Brains, Jesse Kwayu, alisema tafiti zinaonyesha kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, wagombea wanawake walipata nafasi ndogo kwenye vyombo vya habari ikilinganishwa na wanaume, hali inayohitaji kubadilika mwaka huu.
“Tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu, vyombo vya habari vinapaswa kutoa nafasi sawa kwa wagombea wote bila kuonesha upendeleo wa kijinsia,” alisema Kwayu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwenza wa Media Brains na mwandishi mkongwe, Absalom Kibanda, alisisitiza umuhimu wa wanahabari kusoma kwa makini Sheria ya Vyama vya Siasa, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024, pamoja na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
“Sheria hizi zimeanza kutumika kwenye mchakato wa awali wa uchaguzi. Ni muhimu wanahabari wakazifahamu ili kujilinda kisheria na kutekeleza majukumu yao kwa weledi,” alisema Kibanda.
Mkurugenzi wa Media Brains, Neville Meena, aliongeza kuwa uelewa wa sheria utasaidia wanahabari kuepuka makosa, hasa wanapowahoji wagombea na wadau wa uchaguzi.