Wagosi wamrejesha Makambo JR | Mwanaspoti

UONGOZI wa Coastal Union uko katika mazungumzo ya kumsajili aliyekuwa nyota wa Mtibwa Sugar FC na Mashujaa FC, Athumani Masumbuko ‘Makambo Jr’, baada ya mshambuliaji huyo kudaiwa hayupo tayari kuchezea SC Viktoria 06 Griesheim ya Ujerumani.

Nyota huyo alijiunga na 1.FCA Darmstadt Julai 25, 2024 kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Mashujaa aliyojiunga nayo msimu wa 2023-2024, baada ya kuonyesha kiwango kizuri wakati akicheza timu ya vijana ya Mtibwa Sugar U20.

Jina lake lilianza kupata umaarufu mkubwa akiwa na Mtibwa Sugar na aliibuka mfungaji bora wa ligi ya vijana baada ya kufunga mabao saba, huku akiiwezesha pia timu hiyo kutwaa ubingwa kwa kuifunga Geita Gold bao 1-0, Julai 2, 2023.

Hata hivyo, licha ya kujiunga na 1.FCA Darmstadt, mshambuliaji huyo alitolewa kwa mkopo kwenda kuichezea, SC Viktoria 06 Griesheim ya Ujerumani pia, ingawa mambo yamekuwa ni tofauti na sasa anafikiria kurudi tena kuchezea Tanzania.

Kutokana na hilo, mabosi wa Coastal Union ambao mwanzoni kabla ya kwenda Ujerumani walifanya mawasiliano naye, wameingia moja kwa moja kuiwinda tena saini yake, huku ikielezwa mazungumzo yanaendelea vizuri na huenda nyota huyo akajiunga nao.

Chanzo kutoka ndani ya timu hiyo, kililiambia Mwanaspoti viongozi wa Coastal wamempa mkataba nyota huyo ambaye ametaka kuusoma kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho, kutokana na ofa mbalimbali alizonazo kutoka klabu za ndani na nje ya nchi.

“Hatuna shaka na ofa tuliyompa na matumaini yetu atakubaliana nayo, ikiwa atapata nje kama anavyosema tutaridhika kwa sababu lengo letu ni kuona anazidi kupiga hatua zaidi, ila ikiwa ni ndani tutapambana kumpata,” kilisema chanzo hicho.