Wanachosema ndugu wa waliofukiwa mgodini Shinyanga

Shinyanga. Baadhi ya ndugu wa waliofukiwa mgodini wameiomba Serikali iongeze juhudi katika kuwatafuta ndugu zao, huku wakiwa wamejiandaa kwa matokeo yoyote.

Wakizungumza na Mwananchi leo Agosti 15, 2025 katika eneo la tukio la ajali ya mgodi unamilikiwa na Kikundi cha Wachapakazi uliopo katika Kijiji cha Mwongozo Kata ya Mwenge Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ndugu hao wasubiri matokeo.

Mzaliwa wa Kijiji cha Mwomgozo, Ernest Magese ameeleza kuwa ni siku ya tano tangu ajali hii itokee hivyo wanaiomba serikali iongeze kasi ili basi waweze hata kuwatoa ndugu zao walioko ardhini,

“Leo ni siku ya tano tangu ajali hii itokee na tuko hapa tunaomba serikali watu wetu waweze kuwaondoa haraka kwa hali yoyote ile tuwapate hata ndugu zetu,” amesema Magese.

Naye Monica Andrea anasema “Nina kaka zangu wanne humu, tunakaa hapa tunalala hapa tukimuomba Mungu ili basi ndugu zetu waweze kuokolewa, tunaomba sana sana sana,” amesema.

Mkazi wa Misungwi, Mwanza Mrisho Luneleja ameeleza, “Nimekuja hapa kusubiri ndugu zetu ambao wako ardhini wanafanya juhudi za kuwatoa,” amesema Luneleja.

“Nina vijana wangu wawili wako chini tunasubiri hatma ya ndugu zetu kwa wakti huu tumejiandaa kwa lolote kiakili litakalo tokea lakini tu wawatoe huko chini,” amesema Joseph Buzuka.

Ajali hiyo ilitokea Agosti 11, 2025 na kufukia watu 25 ambao walikuwa wakifanya ukarabati wa maduara ya mgodi huo. Agosti 12, 2025 watu wanne waliokolewa na Agosti 13, 2025 mmoja lakini alipoteza maisha wakati anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na hadi sasa watu 21 wako chini ya ardhi.