Arusha. Mahakama Kuu Masijala ndogo ya Tabora imewaachia huru watu wawili Ndugu Pius na Sung’wa Leonard, waliokuwa wameshtakiwa kwa kosa la kumuua aliyekuwa daktari wa mifugo, Cosmas Chalya.
Uamuzi huo umetolewa Agosti 12, 2025 na Jaji Frank Mirindo, wakati akitoa uamuzi iwapo washtakiwa hao wana kesi ya kujibu au lah, baada ya upande wa Jamhuri kumaliza kutoa ushahidi wao.
Jaji Mirindo amesema kuwa hakuna ushahidi wa utambulisho wa awali wa Sung’wa na Hamisi wala gwaride la utambulisho halikufanywa wala hakukuwa na chembe ya ushahidi wa kufanya ungamo la mdomo na kutokana na sababu hizo, anashikilia kuwa washtakiwa hawana kesi ya kujibu kwa mujibu wa kifungu cha 312 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), hivyo kufuta kesi hiyo na kuwaachia huru.
Katika kesi hiyo upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Emmanuel Luvinga huku washtakiwa hao wakiwakilishwa na mawakili Monica Mlaho na Langa Mvuna.
Ndugu na Sung’wa kwa pamoja wanashtakiwa kwa mauaji ya Cosmas, yaliyotokea Mei 28, 2023 katika Kijiji cha Bulumbela, Wilaya ya Igunga mkoani Tabora.
Washtakiwa wote walikana kutenda kosa hilo huku upande wa amshtaak ukiwa na mashahidi tisa na vielelezo vinne.
Shahidi wa kwanza, Punji Pius, alidai kuwa Julai 2023 aliagizwa na Ndugu kupitia simu ya mkononi kuchukua fedha kutoka kwa Said Mageta, kiasi cha Sh800,000 ambapo alipouliza ni fedha za nini alijibiwa ni kwa ajili ya kumuua Cosmas, ila alitakiwa kuficaha siri hiyo.
Aliieleza mahakama kuwa hakuficha siri hiyo na badala yake alitoa taarifa kwa ndugu wa Cosmas na kusababisha washtakiwa hao kukamatwa na kushtakiwa kwa mauaji.
Nakala hiyo inaonyesha kuwa miongoni mwa mashahidi wa upande wa mashtaka walieleza kwamba Cosmas alikuwa daktari wa mifugo wa kitamaduni ambaye alikuwa akienda maeneo tofauti kufanya kazi hiyo.
Ilielezwa kuwa siku ya tukio aliondoka hadi Bujuru kufanya kazi katika Kijiji cha Ngulu wilayani Igunga na kuwa Sung’wa alikuwa mtu wa mwisho kuonekana akiwa na Cosmas akiwa bado hai.
Shahidi wa saba, Hamisi Mang’ola, ambaye alikuwa akifanya kazi katika mashine ya kusaga iliyokuwa inamilikiwa na Cosmas kati ya mwaka 2022 na 2023 alidai kuwa Sung’wa akimchukua Cosmas kwenye pikipiki jioni ya Mei 28, 2023 akielekea kijiji cha Ngulu.
Alieleza kuwa kabla hawajaenda kijijini humo, Cosmas akiwa amebebwa kwenye pikipiki iliyokuwa ikiendeshwa na Sung’wa, alipita eneo la mashine na kukusanya Sh75,000 kutoka kwake kisha wakaondoka.
Shahidi wa nane, Tinginya Andrea, alieleza kuwa Sung’wa alikamatwa na wanamgambo wa eneo la Kijiji cha Bulumbela kuhusiana na muamala wa fedha uliotiliwa shaka kupitia kwa wakala aitwaye Said Ibrahim.
Alidai kuwa alipokamatwa alikiri kupokea baadhi ya fedha kupitia kwa Said na kuwa mtu aliyemchukua Cosmas kwenye pikipiki ili kumpeleka kwa kazi ya Ngulu.
Shahidi wa tatu, Kushoga Lufega na shahidi wa nne, Nkalinyenye Lukala, walieleza kuwachukua wapelelezi na ndugu wa marehemu hadi katika eneo la Kijiji cha Bulumbela na baadhi ya vitu vilitolewa kwenye shimo la kuchimba dhahabu lililotelekezwa.
Walidai miongoni mwa vitu vilivyochukuliwa ni pamoja na cheti cha usajili cha Cosmas kama daktari wa mifugo pamoja na baadhi ya nguo.
Jaji huyo akinukuu mashauri mbalimbali ya Mahakama Kuu na Rufani amesema kuna ushahidi unaoonyesha kifo cha Cosmas, lakini hakuna ushahidi wa wazi wa mawasiliano ya simu ya Ndugu na Punji yanayothibitisha kwamba Ndugu alikiri ushiriki wake katika kumuua Cosmas.
“Hakuna chembe cha ushahidi wa simu halisi za rununu zinazotumiwa na mmoja wao wala nambari zao za simu. Kwa hiyo, hakuna ushahidi wa kukiri kwa Ndugu kumuua Cosmas,” amesema.
“Tena, hakuna ushahidi wa utambulisho wa awali wa Sung’wa na Hamisi wala gwaride la utambulisho halikufanywa, wala kukiri kwa mdomo kwa Sung’wa kwa mgambo hakuwezi kuendeleza kesi ya upande wa mashtaka zaidi,” amesema Jaji.
Jaji amesema kutokana na sababu hizo, anashikilia kuwa washtakiwa hawana kesi ya kujibu kwa mujibu wa kifungu cha 312 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), hivyo kufuta kesi hiyo na kuwaachia huru.
“Kwa mantiki hiyo nafuta shtaka hilo na kumwachia huru mshtakiwa wa kwanza na mshtakiwa wa pili waliokuwa wameshtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu , ” amehitimisha Jaji Mirindo.