ALIYEKUWA mshambuliaji nyota wa Dodoma Jiji, Waziri Junior Shentembo amerejea tena katika timu hiyo baada ya kuondoka kikosini Februari 7, 2025 na kujiunga na kikosi cha Al-Minaa SC kinachoshiriki Ligi Kuu ya Iraq kwa mkopo wa miezi sita.
Nyota huyo alijiunga na Dodoma Jiji kwa mkataba wa miaka miwili, akitokea KMC FC, ingawa ameitumikia kwa miezi sita tu, baada ya kupata dili la kwenda kucheza Iraq, huku kukiwa na kipengele pia cha kumnunua moja kwa moja wakiridhishwa naye.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza Waziri kwa sasa amerejea nchini na tayari amejiunga na Dodoma Jiji kwa lengo la kumalizia mkataba wake wa mwaka mmoja uliobakia, ingawa kukitokea timu inayomhitaji ataruhusiwa kuondoka tena.
“Watu wanapaswa kutambua, Waziri bado ni mchezaji wetu halali kwa sababu alienda Iraq kwa mkopo na endapo wameridhishwa na uwezo wake watamsajili moja kwa moja, kwa sasa ni mapema kusema wazi ataichezea Dodoma Jiji,” kilisema chanzo hicho.
Shentembo hadi anaondoka Dodoma Jiji, alikuwa amefunga bao moja tu la Ligi Kuu Bara katika ushindi wa kikosi hicho wa 2-0, dhidi ya Tabora United, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Oktoba 2, 2024.
Msimu wa 2024-2025, haukuwa mzuri zaidi kwa nyota huyo kutokana na kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara, ingawa msimu bora kwake ni wa 2023-2024, alipokuwa anaichezea KMC aliposhika nafasi ya tatu ya wafungaji, baada ya kufunga mabao 12.
Katika msimu huo, Shentembo alizidiwa na kiungo mshambuliaji nyota wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga mabao 19 na kinara, Stephane Aziz KI aliyekuwa Yanga aliyefunga 21, ingawa kwa sasa anaichezea Wydad Casablanca ya Morocco.
Baada ya kuichezea Al-Minaa SC, mshambuliaji huyo amekuwa ni Mtanzania wa pili kucheza soka la kulipwa katika Ligi Kuu ya Iraq, akifuata nyayo za nyota wa zamani wa kikosi cha Yanga, Saimon Msuva ambaye kwa sasa anaichezea Al-Talaba SC.