BAADA ya JKT Queens kumtambulisha Abdallah Kessy kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, mkufunzi huyo amesema matarajio yake ni kuisaidia timu hiyo katika michuano ya kimataifa na kutetea taji la ndani ililotwaa msimu uliopita katika Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) sambamba na Ngao ya Jamii.
Kessy anarithi mikoba ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Esther Chabruma ‘Lunyamila’, ambaye amepewa mkono wa kwaheri, licha ya kuipatia timu hiyo ubingwa wa Ligi Kuu ambao ulikuwa unatetewa na Simba Queens na ubingwa wa CECAFA.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kessy alisema anafahamu kazi kubwa anayotakiwa kuifanya ndani ya kikosi hicho, hasa michuano ya kimataifa ambayo iko mbele yake kwa sasa.
“Sio mara yangu ya kwanza, kwa sababu nilishawahi kusimamia timu za Umisseta, isipokuwa kwa hapa ni levo kubwa. Najua ugumu wa mashindano ya CECAFA kwa sababu ni timu moja inapaswa kufuzu ukanda wetu wa Afrika Mashariki na msimu mmoja nyuma JKT ilifanya vizuri,” alisema Kessy na kuongeza:
“Matarajio yangu ni kufanya vizuri katika mpira huu wa wanawake kwa sababu hii ndio mara yangu ya kwanza kufundisha Ligi Kuu, na kuanzia katika mashindano yaliyopo mbele yangu.”
Msimu uliopita aliifundisha African Sports ya Tanga, lakini hapo awali alikuwa kocha msaidizi wa Mgambo JKT chini ya Bakari Shime na Sahare All Stars.