Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo katika ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2025 kimeahidi kufanya mageuzi makubwa katika sera za ardhi na rasilimali za Taifa, kikisema wananchi ndio watakaowekwa katikati ya umiliki na manufaa.
Ilani hiyo inabainisha kuwa ardhi ni maisha na msingi wa utajiri wa Taifa, hivyo mageuzi yatakayofanyika yatagusa sekta za ardhi, madini, nishati, uhifadhi na utalii kwa lengo la kuhakikisha rasilimali za Taifa zinawanufaisha Watanzania wote na si wachache au wageni pekee.
ACT-Wazalendo imesema itafuta kile ilichokiita ubinafsishaji holela wa ardhi na kurejesha maeneo yaliyotwaliwa kutoka kwa wananchi bila fidia au ushirikishwaji. Pia, chama hicho kimeahidi kurejesha ardhi ya vijiji iliyogeuzwa kuwa hifadhi na kuwapatia wakulima na wafugaji ili kuondoa migogoro ya muda mrefu.
Ardhi isiyotumika au iliyoachwa wazi itagawiwa kwa vijana na makundi yenye uhitaji ili itumike kuzalisha, huku Tume ya Taifa ya Ardhi ikianzishwa kwa ajili ya kupitia mipaka yote kwa ushirikishwaji wa wananchi.
Kwa mujibu wa ilani hiyo, mfumo mpya wa “Ardhi kwa usawa” utaanzishwa ambao utaruhusu wananchi kumiliki hisa katika miradi ya uwekezaji inayofanyika kwenye ardhi yao. Aidha, ada zote za upimaji ardhi zitafutwa na jukumu la upimaji na utoaji wa hati litabaki kwa Serikali.
Chama hicho pia kimepanga kuweka mipaka ya kiwango cha umiliki wa ardhi, kuweka sharti la matumizi ya hati na kuhakikisha haki za ardhi zinaingizwa kwenye Katiba kwa ulinzi wa kisheria. Umiliki wa kimila utakuwa na hadhi sawa na hati rasmi, huku wageni wakipigwa marufuku kumiliki ardhi.
Kwa upande wa rasilimali, ACT-Wazalendo imesema itabadilisha mfumo wa sasa wa utoaji leseni za madini, mafuta na gesi, badala yake Serikali na wananchi watabaki kuwa wamiliki, huku wawekezaji wakihusika kwa mikataba tu.
Ilani inaeleza mikataba yote ya zamani, ya sasa na inayokuja itakuwa wazi kwa umma na hakuna leseni ya uchimbaji itakayotolewa bila ridhaa ya kijiji husika.
Aidha, chini ya Serikali yake, jamii zilizo jirani na migodi zitapatiwa asilimia 10 ya mrabaha wa madini, huku kampuni zikilazimika kutoa asilimia tatu ya faida zao moja kwa moja kwa jamii hizo.
Chama hicho kimeahidi kupunguza kodi kwa wachimbaji wadogo na kuongeza muda wa leseni zao hadi miaka 10, pamoja na kuharakisha miradi mikubwa ya Mchuchuma, Liganga, Kabanga Nickel na LNG ili kuongeza ajira na mapato ya Taifa.
Kwa upande wa uhifadhi, ACT-Wazalendo kimesema kitaleta mabadiliko makubwa ili kuondoa unyanyasaji unaodaiwa kufanywa chini ya sheria za sasa. Kimeahidi kuvunja Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kuanzisha kampuni itakayomilikiwa kwa pamoja kati ya wananchi na Serikali.
Ilani inasema fidia kwa uharibifu unaosababishwa na wanyamapori itaongezwa hadi Sh2 milioni, huku askari wa wanyamapori wakiongezwa na mbinu mpya kuanzishwa kudhibiti migongano kati ya binadamu na wanyama.
Aidha, chama hicho kimeahidi kusitisha upanuzi wa maeneo ya hifadhi, kuimarisha uhifadhi unaoongozwa na jamii, pamoja na kulinda fukwe, mikoko na matumbawe. Kuta za baharini zitajengwa kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na ubinafsishaji wa visiwa na bahari utakomeshwa.
Kuhusu utalii, chama hicho kimesema kitaondoa mfumo wa sasa wa “package safari” ambapo malipo hufanyika nje ya nchi na badala yake kuanzisha mfumo wa “back-pack safari” ambao malipo yatafanyika ndani ya nchi.
Hoteli zitahitajika kutumia bidhaa za ndani kutoka kwenye kilimo, uvuvi na mifugo kwa kiwango cha asilimia 90, huku utalii vijijini ukihamasishwa na halmashauri za mitaa. Lengo ni kufikisha watalii milioni 10 na kutengeneza zaidi ya ajira milioni 2.5.
ACT-Wazalendo kimesema ajenda ya ardhi na rasilimali si ya kiuchumi pekee bali pia ni msimamo wa kisiasa, kikisisitiza bila kurejesha udhibiti wa ardhi, madini, misitu na bahari, Tanzania itabaki tajiri kwa rasilimali lakini maskini kwa matokeo.
“Rasilimali zetu lazima ziwe baraka kwa kila Mtanzania, leo na kwa vizazi vijavyo,” inaeleza sehemu ya ilani hiyo.
Mchambuzi wa siasa, Dk Paul Loisulie akizungumza na Mwananchi kuhusu ilani ya ACT-Wazalendo, amesema ardhi ni jambo nyeti kwa Watanzania na linahitaji usimamizi mzuri ili kuhakikisha Watanzania wananufaika nayo pamoja na rasilimali zote zilizo ndani yake.
Amesema mataifa mengi ya Afrika yameshindwa kupiga hatua kwa sababu ya usimamizi mbaya wa rasilimali zake, tofauti na mataifa ya magharibi ambayo yalivuna rasilimali zao na kuwekeza kwenye maendeleo ya jamii zao.
“Kweli, ardhi ni eneo muhimu, kama ACT-Wazalendo wameliona inatia moyo kwamba wamejua tatizo lilipo na huo ni mwanzo wa utatuzi wake. Tunahitaji usimamizi mkubwa wa ardhi na rasilimali zetu zote ili tubadilishe maisha ya watu wetu,” amesema.
Amesisitiza kuwa, wananchi watumie fursa ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025 kuchagua viongozi ambao watakwenda kusimamia rasilimali hizo kikamilifu, ili Taifa lipige hatua.
Kwa upande wake, kada wa ACT-Wazalendo, Masoud Shaaban amewapongeza viongozi wake kwa kuja na ilani inayoakisi mahitaji na changamoto za wananchi, akiamini wakipewa ridhaa ya kuongoza Serikali watabadilisha maisha ya watu tofauti na ilivyo sasa.
“Ilani yetu iko vizuri, wataalamu wa chama na viongozi wamekaa na kuja na ilani itakayomkwamua Mtanzania. Niwaombe wananchi, Oktoba wakapige kura na kuzilinda, wasikubali kuibiwa ushindi wao,” amesema.