Anuary Jabir arejea Dodoma Jiji

ALIYEKUWA mshambuliaji wa Dodoma Jiji, Anuary Jabir amerejea tena ndani ya kikosi hicho kwa ajili ya kukitumikia msimu ujao baada ya kumaliza mkataba wake na Mtibwa Sugar aliyoisaidia kupanda Ligi Kuu Bara ikitokea Championship.

Anuary aliyefunga mabao manane katika Ligi ya Championship kwa msimu wa 2024-2025, ameiwezesha Mtibwa Sugar kutwaa taji na kuipandisha baada ya kuongoza na pointi 71, ikiungana na Mbeya City pia iliyomaliza nafasi ya pili na pointi zake 68.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson alisema wanaendelea kufanya maboresho ya timu hiyo kwa lengo la kutengeneza kikosi imara, japo suala la nyota atakayeingia au yule watakayeachana naye wataweka wazi.

“Tumejaribu kufanya maboresho kutokana na mahitaji ya timu ilivyokuwa msimu uliopita, usajili wowote kwa sasa utakaouona tumeachia benchi letu la ufundi lihusike kwa asilimia 100, hivyo tuwe na subra katika kipindi hiki,” alisema Fortunatus.

Hata hivyo, licha ya kauli ya Fortunatus, Mwanaspoti linatambua Anuary aliyeichezea pia Kagera Sugar na KAA Gent ya Ubelgiji aliyoenda kufanya majaribio amekamilisha dili la kurejea Dodoma Jiji na kusaini mkataba wa mwaka mmoja.

Nyota huyo ana kumbukumbu nzuri na kikosi hicho cha Dodoma kwani alikisaidia pia kupanda Ligi Kuu msimu wa 2019-2020, kikitokea Ligi ya Championship huku akionyesha kiwango bora kilichomfanya kuibuka mfungaji bora na mabao 10.