KAMA Mwanaspoti ilivyokujuza juzi ni kwamba Simba wanafanya mambo yao kimyakimya, huku kikosi chao kikiendelea kujichimbia nchini Misri kikibadili mji kutoka ule wa awali kwenda katika jiji kuu la nchi hiyo na mji wa kibiashara maarufu katika Ukanda wa Afrika Kaskazini.
Kikosi cha Simba kimeshahamisha kambi kutoka Ismailia kwenda Cairo ambako hesabu za benchi la ufundi zinaendelea kupigwa ipasavyo, lakini macho na masikio ya wababe hao wa Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam, yaliendelea kufuatilia kila kinachoendelea katika soko la biashara ya wachezaji.
Na unaposoma hapa ni kwamba, inadaiwa kuna baadhi ya nyota wameondoshwa kikosini na matajiri wa timu hiyo wapo sokoni kusaka mbadala wao.
Inadaiwa kuwa Simba bado inaendelea kufanya usajili na inafanya biashara kwa kuuza nyota ambao ofa zao zipo mezani kama inavyoelezwa kuwa mshambuliaji Leonel Ateba muda wowote atatangazwa kupigwa bei kumpisha Naby Camara aliyetambulishwa majuzi.
Simba ipo kwenye hatua za mwisho za mazungumzo ya kufanya biashara ya kumuuza Ateba aliyemaliza msimu kwa kupachika mabao 13, ikielezwa kuwa tayari kocha kapeleka majina mezani ya nyota ambao wanatakiwa kufuatiliwa.
Mwanaspoti tayari lilisharipoti kuwa Simba inafanya mazungumzo na mshambuliaji Privat Djessan Bi ambaye alimaliza msimu uliopita akiitumikia klabu ya Zoman FC ya Ivory Coast na pia wanatupa jicho katika michuano ya CHAN kuona kama watapata nyota atakayeisaidia timu hiyo msimu ujao.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti kuwa, Ateba ameondoka mazoezini kwenda moja ya timu ambayo bado haijajulikani kwa ajili ya vipimo na mambo kama yataenda kama walivyopanga basi timu hiyo imsajili mbadala wake haraka.
“Ni kweli Ateba hatupo naye kambini, lakini taarifa zake zipo na kocha anafahamu kinachoendelea hilo halina shaka ni sehemu ya makubaliano ninachoweza kukuthibitishia kwamba ameenda kufanya vipimo moja ya timu ambayo haijawekwa wazi ila yakienda sawa ndio utakuwa mwisho wake Simba.”
Wakati hayo yakisema hivyo pia inadaiwa, Joshua Mutale pia hatakuwa sehemu ya kikosi atapisha usajili mwingine ndani ya kikosi hicho na taarifa hiyo tayari amepewa wanachoangalia ni kutafuta timu ambayo watamtoa kwa mkopo au kumuuza kama watapata ofa.
Simba tayari imeshavuka idadi ya wachezaji 12 wanaotakiwa kwa mujibu wa kanuni za usajili kwani kwa sasa ina majina 14, ambao ni kipa raia wa Guinea, Moussa Camara, mabeki Chamou Karaboue (Ivory Coast), Rushine de Reuck (Afrika Kusini) na Naby Camara.
Pia kuna viungo Neo Maema anayesubiri utambulisho kutoka Afrika Kusini, Allasane Kante (Senegal), Mkenya Mohamed Bajaber, Mzambia Joshua Mutale, Mkongomani Ellie Mpanzu, Jean Charles Ahoua, Jonathan Sowah, Steven Mukwala na Ateba, huku ikielezwa dili la Hernest Malonga huenda limekufa baada ya kutua kwa Naby Camara, japo aanendelea kuangaliwa mazoezini.
Hata hivyo, taarifa nyingine zinasema kuna uwezekano Joshua Mutale akaondoka kikosini kwa dili zilizopo mezani kwa mabosi wa Simba kama ilivyo kwa Ateba, Steven Mukwala na Jean Charles Ahoua, hivyo kumrahisishia usajili mwingine.
Mwanaspoti ilifanya juhudi za kumtafuta Malonga ili kuzungumzia dili lake na Simba alisema yeye sio kazi yake kuzungumza watu sahihi wa kufanya hivyo ni viongozi wa timu lakini yeye bado anaendelea na mazopezi.
Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema bado hawajamaliza kusajili wanaendelea kufanya hivyo lakini hafahamu taarifa za kuondoka kambini kwa wachezaji hizo hazijamfikia mezani kwake na kuhusu Malonga pia alisema hana taarifa.
“Mpya nilizonazo ni Naby Camara kupewa mkataba wa miaka miwili kuitumikia Simba mambo mengine naomba kupewa muda kwa sababu siwzi kuyatolea ufafanuzi wakati mezani kwangu hayajafika ila bado tunafanya usajili,” amesema mchezaji huyo.