MSHAMBULIAJI wa timu ya taifa ya Guinea, Ismael Camara amewaomba radhi mashabiki wa timu hiyo kufuatia sare ya kufungana bao 1-1 na Algeria iliyowaondoa kwenye nafasi ya kuwania kufuzu robo fainali ya Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Guinea chini ya kocha Souleymane Kamara ilitangulia kupata bao kupitia kwa Camara dakika ya 61. Zikiwa zimesalia dakika nane kumalizika, Soufiane Bayazid wa Algeria alisawazisha na kuzima matumaini ya timu hiyo kucheza robo fainali.
“Tulihitaji ushindi ili kubaki kwenye mbio, lakini dakika nane kabla ya kumalizika tukaruhusu bao la kusawazisha. Tulikuja kushinda, tulijitahidi, lakini tumeondolewa hatua ya makundi jambo ambalo halikuwa lengo letu. Natoa samahani za dhati kwa taifa zima la Guinea,” alisema Camara.
Kocha wa Guinea, Kamara, alisema: “Tumecheza kila baada ya siku tatu bila mapumziko. Hilo limetuathiri kwa kiasi kikubwa. Pia, unahitaji kuchukua hatari, na labda hatukuwa jasiri vya kutosha kwenye mashambulizi.”
“Unapofungwa ukiwa uwanjani, hakuna nafasi ya kulaumu mambo ya nje. Tunapaswa kufanya kazi kwa mfumo thabiti, kama zilivyo timu nyingine za Afrika zilizoko mbele yetu kwa sasa.”
Kwa upande wa kocha wa Algeria, Magid Bougherra alisema licha ya kuwa bado ana mechi ya mwisho kuamua hatma ya kusonga mbele dhidi ya Niger, alikiri bado kikosi chake kina mapungufu hasa eneo la umaliziaji.
“Ilikuwa mechi ngumu, kwenye uwanja mgumu. Tulikosa nguvu za mwili na ufanisi wa kumalizia. Tulipata nafasi za kufunga na kushinda mchezo lakini hatukuzitumia. Katika soka la ndani la Afrika, kumalizia mashambulizi bado ni eneo linalohitaji maboresho.”
“Kama tunataka kufuzu, tunapaswa kushinda mechi ijayo dhidi ya Niger. Hatma ipo mikononi mwetu, ingawa sio mechi rahisi kwa sababu timu hiyo haitakuja kucheza kumaliza tu ratiba, naamini itaonyesha upinzani mgumu.”