DKT. KIMAMBO AFANYA ZIARA KITUO CHA TIBA KAZI NA UTENGAMAO WA AFYA YA AKILI (VIKURUTI)

::::::::

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Delilah Kimambo leo Agosti 16, 2025 amefanya ziara Kijiji cha Tiba Kazi na Utengamao wa afya ya akili (Vikuruti) ambacho ni sehemu ya hospitali hiyo ili kuzungumza na watumishi, kuona utendaji kazi na kujadili njia bora za kuboresha huduma na utendaji kazi.

Akizungumza na watumishi katika kijiji hicho kilichopo Chamanzi, Temeke, Jijini Dar es salaam amewapongeza kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya na kuelekeza maboresho ya miundombinu ili kuendelea kupeperusha vyema bendera ya hospitali.

“Hongereni sana kwa kazi nzuri mnayofanya na kwa moyo wa kujituma kitu kinachofanya Kijiji hiki kuendelea kuwa bora,naombeni muendeleze moyo huo na mboreshe zaidi miundo mbinu ili huduma iiendelee kwa ufanisi zaidi,” amesema Dkt. Kimambo.

Ziara hiyo ambayo ni ya kwanza kwake kutembelea kijijini hapo pia imeangazia ujenzi wa mradi mpya wa Vikuruti unaotarajiwa kuanza hivi karibuni kwa ushirikiano kati ya hospitali na muwekezaji .