MSHAMBULIAJI wa Mauritania, El Mami Tetah amefichua kwamba licha ya kupoteza mbele ya Taifa Stars katika mechi ya kundi B, mshikamano wa kikosi chao umewawezesha kumaliza makundi wakiwa na pointi saba.
Mauritania ilipoteza mechi moja, ikitoa sare moja na kushinda mbili – matokeo ambayo yameifanya ishike nafasi ya pili kwenye msimamo kabla ya mechi za jana usiku, ambapo Burkina Faso yenye pointi tatu ilicheza dhidi ya Madagascar yenye alama nne. “Kundi letu halikuwa rahisi hata kidogo. Tulicheza dhidi ya timu zenye uwezo mkubwa wa ushindi, ikiwemo wenyeji Tanzania na wapinzani wengine wenye uzoefu mkubwa,” alisema Tetah.
Tetah, ambaye alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi dhidi ya Burkina Faso Jumatano iliyopita, aliongeza: “Ushirikiano wa wachezaji, nidhamu, na utendaji wa kila mmoja ulichangia kukusanya pointi ambazo tumepata. Hii ni ishara kwamba timu yetu inakua kila siku.”
Mbali na mechi ya Burkina Faso na Madagascar, ambayo ilikuwa vita ya kusaka nafasi ya pili kwenye kundi hilo, Mauritania ilipata changamoto kubwa kutoka Taifa Stars na kupoteza kwa mabao 2-1.
Akiizungumzaia Stars, Tetah alisema: “Naweza kusema ndio timu iliyotusumbua zaidi. Kupoteza dhidi yao kulitupa sababu ya kupambana zaidi katika mechi zilizoendelea mbele yetu. Ilituumiza kichwa, lakini pia ilitufundisha mengi.