Hekaya za Mlevi: Akili mnemba kizibo cha akili

Dar es Salaam. Zamani tulikuwa tunatumia tembe dhidi ya malaria zilizojulikana kama “kwinini”. Tembe hizi zilikuwa chungu kiasi kwamba mgonjwa alizihisi mpaka kisogoni pale alipozimeza. 

Wagonjwa wengi walikuwa wakizitupia uvunguni, ndipo wataalamu wakabuni njia ya kuwavutia. Wakaziweka tabaka la utamu uliofanana na ule wa peremende. Angalau kwa njia hii wagonjwa walishawishika kuzitumia.

Lakini tabaka lile lilikuwa jembamba sana. utamu ulibaki kwa muda mfupi sana kabla haujakatika. Kama ungejisahau na ladha yake na ukaziacha dawa mdomoni kwa sekunde chache, utamu uliisha na ghafla ungeisikia shubiri yake. Matokeo yake ungezitema na zingezidi kukukereketa. Hata hivyo ilisaidia hasa kwa watoto kumeza vidonge vile, maana bila hivyo mgonjwa angeweza kuteseka kwa siku nzima.

Muziki wa zamani ulikuwa kama kidonge cha kwinini. Ulitoa ujumbe wa kweli juu ya maisha ya watu bila kujali ni mchungu kiasi gani. Lakini ili kuwavutia wasikilizaji, uliwekwa ladha tamu kupitia ala na sauti. Kwa njia hii kila mmoja alishawishika kuusikiliza hata kama mashairi yake yalimnanga msikilizaji. Wapenzi wa muziki walisafiri huku na huko kuzifuata bendi zao, wakaucheza huku ujumbe ukiwaingia.

Widegren ni daktari mtaalamu wa magonjwa ya sikio, pua na koo kutokab Sweden. Alifikiria kwamba hata angalifanya matangazo makubwa kwa kiasi gani, asingewafikia walengwa kwa wingi na urahisi kama alivyokusudia. Akabuni njia ya kuuweka ujumbe wake wa tiba kwenye muziki na tamthilia. Kwenye miaka ya 90 alikuwa mmoja wa waigizaji wakuu katika kundi maarufu la Lundaspexarna.

Hakuishia hapo. Katika vijana wa zamani, hakuna anayeweza kusahau tamthilia ya Shaka Zulu. Basi kwenye tamthilia hiyo, Widegren ameshiriki vikubwa ambapo mwaka 1998 alikuwa meneja katika sehemu ya maonesho yake. Aliingia zaidi kwenye muziki pale alipotoa ngoma ya “Never Google Your Symptoms”. Video ya wimbo huo ilisambaa na kutazamwa zaidi ya mara milioni 5 kwenye mtandao wa YouTube.

Hapa ndipo ninaposhawishika na dhana ya kumfuata mteja katika matamanio yake. Watu hawapendi shuruba, ila kula bata na kujiachia. Iwapo una ujumbe wa kuwashauri watu kuachana na ngono, uweke kwenye burudani halafu wapelekee hukohuko klabu. Wimbo 
“Never Google Your Symptoms” uliimbwa kwa utani na tahadhari dhidi ya watu wavivu wasiopenda kuchunguza afya zao. Wengi walibweteka kwa kuchunguza afya zao mitandaoni.

Lengo lilikuwa kuelimisha kwa njia ya burudani. Tabia ya kutafuta dalili za afya yako kwenye Google huweza kukupa matokeo yasiyo sahihi kwa namna mbili kukufikisha kwenye majibu ya kutisha yatakayokuanzishia taharuki na msongo, au kukupa majibu rahisi ambayo yatazidi kukuangamiza. Yote haya ni mapambano ya kumwokoa mwanadamu, asije akakabidhi maisha yake kwa mashine na kuishi kama roboti.

Kwa mfano umegundua kipele kwenye sehemu ya tumbo lako, “ukagugo” mitandaoni. Majibu yanaweza kurudi “una saratani ya utumbo” au “gonjwa la hatari” hata kama una kijipu uchungu tu. Ukurasa mwingine utakujibu “una kijipu uchungu” hata kama una saratani. Daima mbwa hupokea amri kutoka kwa bwana anayemfuga, hivyo akili mnemba haziwezi kuwa na akili kuliko watu wanaozitengeneza.

Tatizo ni watu wangapi wanaozihuisha programu za akili mnemba. Na ni kwa kiasi gani tunawaamini kushika funguo za akili zetu. Kama nilivyotangulia kusema pale mwanzoni, watu wa sasa hawapendi kushughulisha akili zao, kila kitu kinarahisishwa na kutafutiwa kitegemezi badala yake. Tangu kugundulika kwa kikokotoo, hakuna tena anayejishughulisha na hesabu za vidole wala kichwa.

Mtu mwenye ukwasi, maendeleo na anayekwenda na wakati ni yule anayetumia mifumo ya robot, alarms na kamera za ulinzi nyumbani. Ni yule ambaye trei ya mayai kwenye jokofu ikiisha, jokofu linatoa taarifa kwa wakala ili aje kulijazia. Tena ni yule ambaye kila anapoamka asubuhi anapima uzito na kucheki afya yake kwenye kompyuta ya familia. Wenyewe tunasema hayo ndiyo maisha ya kisasa!

Maisha ya kizamani yalikuwa na uhalisia sana. Mwalimu alitoka nyumbani saa 12 asubuhi na kuanza kazi saa 2. Saa nne angefungua kinywa na kula chakula cha mchana saa saba. 
Ilipofika saa 11 alimaliza kazi na kurudi nyumbani. Kutoka hapo alikuwa na saa nne mpaka tano ya kuongea na familia ama kustarehe kidogo. Wakati ule tulikuwa tukilala angalau kwa saa nane kila siku, muda unaotosha kupumzisha mwili na akili.

Kijijini mkulima angetoka saa 10 alfajiri. Angeipiga ngwe yake hadi saa tano, angeng’oa muhogo na kuugegeda. Hapo angepiga ndefu hadi saa 12. Wakati ndege wanarudi viotani, naye angerudi msongeni mwake. Hivi sasa binadamu hana muda wa kulala wala kuamka bali huamshwa na alarm. Anakula kwa kengele kwani hana hata muda wa kuhisi njaa. Hana muda wa kuongea na familia, kwani mwenza yupo bize na watoto kwa “Sir” au “Madam” shuleni.

Nimegundua kuwa ubishi niliouanzisha sio wa kitoto, lakini wengi hudhani kufia vitani ndio “kufa kishujaa”. Walimwengu walisema “Akimbiaye vita si askari mwoga, bali ni shujaa anayekwenda kujipanga kwa ushindi”. Na mimi acha nikajipange ili nirudi tubishane vizuri. Tuonane wiki ijayo!