Jeshi la Magereza latangaza ajira kwa vijana, omba hapa

Dar es Salaam. Jeshi la Magereza limetangaza nafasi za ajira kwa vijana wa Kitanzania wenye elimu ya kuanzia kidato cha nne na wenye ujuzi katika fani mbalimbali kuanzia ngazi ya stashahada hadi shahada.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Kamishna Jenerali wa Magereza, Jeremiah Katungu leo Agosti 15, 2025, vijana watakaokidhi vigezo watapaswa kuomba kupitia mfumo wa ajira wa Jeshi la Magereza (TPSRMS) kupitia tovuti ya https://ajira.magereza.go.tz.

Mwisho wa kupokea maombi hayo ni Agosti 29, 2025.

Aidha, waombaji wanatakiwa kuwa raia wa Tanzania, wenye umri kati ya miaka 18 hadi 24 kwa waliohitimu kidato cha nne, na miaka 18 hadi 28 kwa wenye ujuzi wa kitaaluma.

Pia, wanatakiwa kuwa na afya njema, nidhamu na tabia njema, wasio na alama za miili (tattoo), na wasiokuwa na rekodi ya makosa ya jinai.

Vilevile, waombaji wanapaswa kuwa na urefu usiopungua futi 5.4 kwa wanawake na futi 5.7 kwa wanaume, wawe tayari kuhudhuria mafunzo ya awali ya askari magereza na kufanya kazi popote Tanzania Bara.

Miongoni mwa fani zinazotajwa ni Uhandisi wa Programu, Sayansi ya Habari Mseto, Usalama wa Mifumo (Cyber Security), Uhandisi wa Mitandao, Saikolojia na Ushauri Nasaha, Uhandisi wa Uchimbaji Madini, pamoja na stashahada katika taaluma za Uuguzi, Ufundi wa vifaa vya ofisi, Lugha za Alama, Kilimo, Mifugo, na Katibu Muhtasi.

Jeshi la Magereza limeonya kuwa mwombaji yeyote atakayewasilisha nyaraka za kughushi au kuficha sifa za kitaaluma atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Hata hivyo, wale waliowahi kufukuzwa mafunzo ya awali ya askari magereza hawaruhusiwi kuomba tena.