Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imeadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, ikieleza mafanikio yaliyofikiwa katika sekta ya afya, yakiwamo kupunguza utegemezi wa matibabu ya moyo nje ya nchi na kuongeza mapato ya Taifa kupitia tiba utalii.
Maadhimisho hayo yamefanyika leo Agosti 15, 2025 katika Ukumbi wa Maktaba Mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), yakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe.
Kabla ya kuanzishwa taasisi hiyo mwaka 2015, Serikali ilikuwa ikitumia Sh554 bilioni kila mwaka kupeleka wagonjwa wa moyo nje ya nchi kwa matibabu.
Dk Shekalaghe amesema mafanikio ya JKCI ni matokeo ya sera na mikakati madhubuti ya Serikali kupitia Wizara ya Afya, ikiwa ni pamoja na uwekezaji mkubwa katika miundombinu, mafunzo ya wataalamu na usimamizi wa hospitali za rufaa.
“Wizara imeweka mkazo katika kusogeza huduma kwa wananchi kwa kujenga hospitali, zahanati na vituo vya afya kote nchini. Hili limepunguza kwa kiasi kikubwa usumbufu wa kwenda mbali kutafuta huduma za afya,” amesema.

Mafanikio hayo pia yamewezeshwa na uwekezaji katika rasilimaliwatu kwa kutoa mafunzo kwa madaktari bingwa na wabobezi katika fani mbalimbali, ikiwamo ya tiba ya moyo.
Balozi John Ulanga, ambaye ni Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amesema uwekezaji wa Serikali katika taasisi kama vile JKCI, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) umefanya Tanzania kuwa kitovu cha matibabu kwa nchi jirani.
“Kuanzia mwaka 2021 hadi 2025 idadi ya wagonjwa kutoka nje ya nchi waliopatiwa huduma JKCI imeongezeka mara mbili kutoka 5,705 hadi kufikia 12,180,” amesema na kuongeza:
“Kupitia mpango wa Dk Samia Outreach nchini Comoro, Serikali ilitumia Sh300 milioni na kufanikisha mapato ya Sh2 bilioni, jambo linaloonyesha faida ya uwekezaji wa afya kama nyenzo ya kiuchumi.”
Amesema wagonjwa wa kimataifa wanatoka nchi 16 barani Afrika zikiwamo Comoro, Burundi, Zambia, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Utalii Tiba, Abdulmalik Mollel, amesema JKCI imekuwa mfano wa mafanikio ya huduma za matibabu ya moyo ikitoa zenye viwango vya kimataifa vinavyowavutia wagonjwa wa kimataifa.
“JKCI imekuwa ikihudumia idadi kubwa ya wageni kutoka nje ya nchi, miaka michache iliyopita sisi ndio tulikuwa tunakwenda kutafuta huduma za tiba ya moyo nje, leo wenzetu ndio wanakuja kwetu, hili ni jambo la kujivunia,” amesema.
Ameishauri Serikali kuongeza msukumo katika kukuza tiba utalii kama eneo la kimataifa la kiuchumi kama ilivyo kwenye sekta nyingine za utalii hifadhi na fukwe.
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema walipofika ni kutokana na bidii, mikakati madhubuti ya Serikali na kuanzishwa kwa kamati maalumu zilizopelekwa kujifunza kutoka taasisi zilizoendelea nje ya nchi.
“Siri ya mafanikio yetu ni kazi kwa bidii na kujitoa, tulianza kwa kuwafuata wananchi mtaani tukawapatia elimu juu ya magonjwa ya moyo, tukajenga imani ya Serikali, ikatupa usaidizi mkubwa na matokeo ndiyo haya,” amesema.