Muda mfupi baada ya kuchaguliwa kwa kishindo kuendelea kuliongoza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), rais Wallace Karia amesema hawana muda wa kulipa kisasi.
Karia akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufunga mkutano wa uchaguzi huo ambao umefanyika katika Hoteli ya Tanga Resort mjini humo amesema licha ya uongozi wake kupitia nyakati ngumu, lakini hawatalipa kisasi.
Karia amesema uongozi wake hautafanya mambo ya kulipa kisasi ambapo watajipanga kufanya mambo ya maendeleo kwa maslahi ya soka la Tanzania.
“Tuna jukumu kubwa la kuhakikisha tunaendelea kupiga hatua za kimaendeleo. Tanzania tunaendelea kukua kwa kasi sana nadhani tutajikita huko,” amesema Karia.
“Tutawataka wadau wetu kufuata utaratibu na kanuni, tutakwenda kubadilisha kanuni mnbalimbali kama ambavyo wadau wametoa mapendekezo.
“Tutakwenda kuipa nguvu Bodi ya Ligi hatutataka tena lawama kwa TFF. Sisi TFF tutatabaki kusimamia mambo makubwa ya utawala na maboresho ya kanuni.”