KIPA wa timu ya taifa ya Niger, Mahamadou Kassali amesema walipaswa kushinda dhidi ya Afrika Kusini mechi ya Kundi C kwani walipata nafasi tatu za kufunga lakini walikosa kuzitumia.
Mchezo huo uliopigwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela na kumalizika kwa sare tasa umeiondoa Niger kwenye mbio za kufuzu robo fainali baada ya kukusanya pointi moja na kushika mkia, huku Afrika Kusini ikifikisha jumla ya pointi tano katika nafasi ya tatu.
Licha ya Niger kuondolewa mapema kwenye michuano, Kassali alionyesha kiwango bora kwa kuokoa mashuti matano ya hatari ya Bafana Bafana na kuibuka na tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi.
“Nimeridhishwa sana na matokeo ya michezo yetu miwili ya kwanza, tulikuwa na uchovu kidogo lakini angalau tumeanza kuzoea,” alisema Kassali na kuongeza:
“Tulipata sapoti kubwa kutoka kwa benchi la ufundi, lakini tulipaswa kupigania sisi wenyewe. Bahati nzuri nikapata tuzo ya Mchezaji Bora, lakini tuna mechi ya mwisho dhidi ya Algeria naamini itakuwa mechi nzuri.”
“Tulihitaji kushinda mechi hii, na kama tungeshinda dhidi ya Afrika Kusini, naamini tungelikuwa na nafasi ya kufuzu kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Algeria. Ni bahati mbaya lakini ndivyo mpira ulivyo.”
Kundi C bado lipo wazi licha ya wenyeji Uganda kuongoza wakiwa na pointi sita, kwani hawajafuzu na wanahitaji ushindi dhidi ya Afrika Kusini, ambayo nayo inahitaji matokeo chanya ikiwa na pointi tano.
Wakati huohuo, Algeria ipo kwenye nafasi nzuri ya kufuzu kwani inahitaji sare tu dhidi ya Niger ambao tayari wametolewa ili kutinga hatua inayofuata.