Kitimwendo charejesha tabasamu la mtoto Hussein

Tabora. Mtoto Hussein Abdala Mkomwanzoka ni mtoto mwenye umri wa miaka 7 mkazi wa Kijiji cha Ndevelwa, Kata ya Ndevelwa Manispaa ya Tabora ambaye amekabidhiwa baiskeli ili kumuwezesha kufika shuleni na hiyo ni kwa sababu ya  ulemavu wa miguu ambao pia imekuwa sababu ya kushindwa kuhudhuria vyema masomo yake.

Amesema amefarijika kupata baiskeli kwani awali ilikuwa mpaka abebwe au kujiburuza mpaka afike shuleni hivyo ilikuwa inasababisha wakati mwingine akiwa amechoka haendi shuleni.

“Mwanzo nilikuwa mtoro sana shuleni kwa sababu kujiburuza nachoka sana, lakini sasa hivi nina furaha na namshukuru Mkurugenzi John Pima kwa kuninunulia baiskeli lakini unaona kama hivi nchi yetu ina amani na nampenda sana Mama Samia Suluhu Hassan, basi nataka nisome sana ili nikiwa mkubwa niwe mwanajeshi niongeze ulinzi zaidi,” amesema.

Bibi wa Husein akizungumza na mwandishi wa habari alipomtembelea nyumbani kwake. Picha na Hawa Kimwaga

Mkuu wa Shule ya Msingi Ndevelwa, John Paul Nsunya amemwelezea Husein kwamba ni mtoto anayependa kujifunza na maendeleo yake darasani ni ya wastani licha ya kuwa awali alikuwa na mahudhurio yasiyoridhisha.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora,  John Marco Pima baada ya kupata taarifa za mtoto huyo kupitia chombo cha habari cha Mwananchi, amenunua baiskeli kwa ajili ya Husein na kwamba halmashauri inaandaa mpango maalumu wa kuwatambua watoto wenye ulemavu ili kuwasaidia kufikia ndoto zao.

“Ninaamini kuwa watoto wenye changamoto ya ulemavu kama Husein ni wengi huko kwenye jamii ni vile tu hawajafikiwa, hivyo lazima tuwatambue hata wale wanaofichwa ndani wajulikane watolewe wapate haki ya elimu,” anasema mkurugenzi.

Salma Miyombo ambaye ni bibi wa Husein ameishukuru Serikali kupitia na kueleza kwamba familia hiyo imefarijika kwani hali yao ya maisha ni duni, hivyo hawakujua ni lini wangeweza kumnunulia baiskeli kama hiyo.

“Sina cha kusema kabisa kwa furaha niliyo nayo mimi na familia yangu, baba wa mtoto hatupi ushirikiano na alimuacha mtoto wetu baada ya kuzaliwa kutokan na ulemavu,” amesema.

Mkazi wa Kata ya Ndevelwa, Jalala Iswaga amesema mara nyingi katika jamii hasa vijijini kwao mtu akijifungua mtoto mwenye ulemavu familia inaona kama ni mkosi ndiyo maana huwa watoto wa aina hiyo huwa wanatelekezwa.