KOCHA wa Algeria, Madjid Bougherra, ametuma ujumbe mzito kwa wachezaji wa ndani akiwemo nyota wa Taifa Stars, Feisal Salum Fei Toto na Clement Mzize, akisisitiza kuwa vipaji vya Afrika ndiyo uti wa mgongo wa soka la Ulaya na kinachohitajika ni kujiamini na kufanya kazi kwa bidii ili kufikia mafanikio makubwa.
Bougherra, aliyewahi kuwa beki tegemeo wa timu ya taifa ya Algeria, amesema wachezaji wengi wanaong’ara kwenye ligi kubwa duniani wametokea barani Afrika, jambo linaloonyesha ubora uliopo kwenye mashindano ya ndani kama CHAN 2024.
Amewataka vijana wasipuuze nafasi ya kucheza katika ligi zao za nyumbani, kwani ndiko ndoto zao zinaweza kuanzia kabla ya kupiga hatua kubwa zaidi.
“Amini katika ndoto zako. Fanya kazi kwa bidii, boresha kiwango chako kila siku. Vipaji vya Afrika ndivyo vinavyoendeleza soka la Ulaya na kila kijana anaweza kufika pale anapopataka,” alisema Bougherra. Akizungumzia CHAN ya mwaka huu, kocha huyo alisema kiwango kimepanda na ushindani ni mkubwa kuliko miaka ya nyuma, huku timu nyingi zikionekana zikiwa na uwezo wa kupambana hadi hatua za mwisho.
Kwa maelezo yake, maendeleo haya yamechochewa na uwekezaji katika akademi na programu za kukuza vijana ambazo zimekuwa chanzo cha wachezaji wengi kuibuka na kupata nafasi ya kucheza soka la kimataifa. Bougherra, aliyeiongoza Algeria kufika fainali ya CHAN 2023 nyumbani, amesema historia si kigezo cha mafanikio ya sasa.
“Tunapaswa kuangalia tulipo sasa na tunapoelekea, si tulipotoka. Hii ni safari mpya,” alisema.
Algeria ya Bougherra imeanza vizuri mashindano haya kwa kuichapa Uganda 3-0 kisha kutoa sare ya 1-1 na Afrika Kusini, kabla ya jana, Ijumaa kuivaa Guinea iliyopoteza mechi mbili mfululizo.