Kocha Yanga ampa kazi maalumu staa mpya

SIKIA pale Yanga kuna mafundi kadhaa wametua katika dirisha hili la usajili, huku pia wakitua kikosini na kocha mpya, Folz Romain aliyerithi mikoba ya Miloud Hamdi aliyetimkia Ismaily ya Misri mara tu baada ya kuibebesha ubingwa wa Ligi Kuu bara msimu uliopita.

Na kama unafuatilia, jana jioni kikosi cha Yanga kilikuwa uwanjani jijini Kigali kuvaana na Rayon Sports ya Rwanda katika mechi ya kirafiki ya kimataifa na tayari umejionea mwenyewe namba mafundi wapya waliotua Jangwani wanavyoupiga mwingi.

Lakini ndani ya kikosi hicho kuna straika mmoja mpya aliyetua hivi karibuni, Andy Boyeli amekiri kupewa kazi maalumu na kocha Folz kitu ambayo ni kama mtego kwake.

Straika huyo aliyetua Jangwani kwa mkopo kutoka Afrika Kusini, amezungumza na Mwanaspoti na kufichua kocha huyo amezungumza naye na kumpa maelekezo ya kitu cha kufanya kutokana na timu hiyo kuwa na viungo na washambuliaji wenye viwango, hivyo ana kibarua cha kuchuana nao.

Boyeli aliyesajiliwa na Yanga katika dirisha hili akitokea Sekhukhune ya Afrika Kusini akipewa mkataba wa miaka miwili, huku akiwa na rekodi ya kufunga mabao sita msimu uliopita ameliambia Mwanaspoti kuwa ni furaha kwake kujiunga na timu kubwa yenye historia ya kuchukua ubingwa mfululizo Bara, lakini ni wazi kuwa ana kazi ya ziada.

Amesema hawezi kuacha kuanza kuwasifu wachezaji wenzake aliowakuta hasa katika eneo la kiungo na ushambuliaji ambao anafanya nao kazi kwa karibu uwanjani.

“Nimefurahishwa na namna nilivyopokewa ndani ya timu hii, lakini kitu kilichonikosha zaidi ni namna kikosi kilivyo na kinavyocheza… kweli wanacheza mpira mkubwa unaweza ukaogopa,” amesema na kuongeza:

“Timu ina viungo wengi na washambuliaji wenzangu niliowakuta wamefanya kazi kubwa na hata mimi najua natakiwa kuendeleza zaidi pale walipoishia kwani malengo ya timu ni makubwa na bado hayajaisha.”

Mkongomani huyo ameongeza zaidi kuwa kocha wa timu hiyo amemtaka ajipange ili kuweka rekodi ya kufunga mabao mengi ndani ya kikosi cha Yanga.

“Kocha ameniambia ndani ya Yanga hakuna kizuizi cha kufunga kwa sababu mshambuliaji anapata kila huduma kutoka kwa mastaa waliopo hasa viungo Ameniambia natakiwa kujipanga kuweka rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi ndani ya timu hii ili kuhakikisha historia nzuri iliyonayo Yanga inazidi kuendelea msimu ujao,” amesema Boyeli aliyetua Jangwani na mzuka.

Mwanaspoti liliwahi kwenda kwenye mazoezi ya kikosi hicho na kujionea uwezo wa Mkongomani huyo mwenye nguvu na akili ya kufunga akiwatesa makipa wa timu hiyo.

Tangu atue Yanga amekuwa akionyesha uwezo wa kufunga mabao ya nje ya eneo la hatari pia yale ya ndani ya eneo la hatari, huku akionyesha kuwasumbua mabeki wa timu yake kwa nguvu zake akiwa na mpira.

Boyeli katika nafasi anayochezea ndani ya Yanga yupo na mastaa ambao walimaliza msimu uliopita wakiwa na rekodi bora za ufungaji katika timu walizotoka, huku wengine wakiwa ndani ya kikosi hicho. Offen Chikola kutoka Tabora United (mabao 8), Celestine Ecua aliyetokea Asec Mimosas (15), Prince Dube (13) na Clement Mzize (14) waliokuwapo msimu uliopita ndani ya kikosi hicho pamoja na Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli.