Madagascar yaifumua Burkina Faso ikiifuata Stars robo fainali

TIMU ya taifa ya Madagascar imeungana na Taifa Stars kutinga robo fainali ya mashindano ya CHAN, baada ya kuifunga Burkina Faso mabao 2-1, kwenye Uwanja wa New Amaan Stadium, Zanzibar.

Matokeo hayo yameifanya Madagascar kuizidi kete Mauritania iliyokuwa ikishika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi B, kabla ya Madagascar kuibuka na ushindi huo muhimu wa kuwavusha.

Madagascar imefungana pointi na Maurtania zote zilikusanya pointi saba lakini imebebwa na idadi ya mabao na imefunga mabao matano na kufungwa matatu, wakati Maurtania imefunga mawili na kufungwa moja.

Madagascar ilianza kuandika bao lake la kwanza dakika ya saba ya mchezo nakabla ya wapinzani wao kusawazisha dakika ya 24, mabao yaliyodumu hadi kipindi cha kwanza kinatamatika.

Mchezo ulianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu lakini Madagasca ilionekana kuwa na uhitaji zaidi kutokana na juhudi za kuliandama lango la wapinzani na kupachika bao hilo la mapema, likifungwa na Fenohasina Gilles, huku la Burkina Faso likifungwa na Souleymane Sangare.

Kipindi cha pili timu zote mbili ziliingia kwa kushambuliana mara kwa mara na makosa ya safu ya ulinzi ya Burkina Faso yaliinufaisha Madagasca kwani ilipata faida ya penati dakika ya 58, iliyofungwa na Nomena Rafanomezantsoa.

Bao hilo ni kama liliizindua Burkina Faso ambayo ilionyesha kupambana zaidi ili kupata bao la kusawazisha, lakini uimara wa safu ya kiungo cha ukabaji na beki ya Madagasca uliizuia kupata nafasi ya kupenya.

Kwa ushindi, Madagascar inaungana na Tanzania kufuzu hatua ya robo fainali kundi B, ikikusanya pointi saba, pointi tatu nyuma ya Taifa Stars  iliyovuna pointi 10 baada ya ushindi wa mechi tatu na suluhu moja.