Mahakama yakataa shauri la mwanahabari aliyeutaka urais TFF

Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, leo, Jumamosi, Agosti 4, 2025 imekataa kusikiliza shauri lingine lililokuwa limefunguliwa dhidi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) kuhusiana na uchaguzi wake mkuu.

Uchaguzi Mkuu wa TFF umefanyika leo Jumamosi, Agosti 16, 2025, jijini Tanga, ambapo Wallace Karia amechaguliwa tena kuwa rais wa TFF kwa muhula wa tatu.

Katika uchaguzi huo Karia alikuwa mgombea pekee baada ya washindani wake waliojitokeza kuchukua fomu kutenguliwa kwa kukosa sifa kuungwa mkono na wajumbe wasiopungua watano (endorsements) ambao wote kasoro mmoja  walikuwa upande wake.

Wakati uchaguzi huo unafanyika Tanga, jijini Dar es Salaam kulikuwa na shauri ambalo pia lilikuwa kinaendelea kuhusiana na uchaguzi huo lililokuwa limefunguliwa na na mwanahabari Ally Thabiti Mbingo.

Mbingo ambaye ana ulemavu wa macho, amewahi kunukuliwa na vyombo vya habari kuwa baada ya kuchukua na kuirejesha fomu hiyo, hakuwahi kuitwa wala kupewa mrejesho tena na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuhusu kilichoendelea, hadi aliposikia kuwa amepitishwa Karia mgombea pekee.

Kupitia Wakili wake Cletus Nziku alifungua shauri dogo la maombi ya zuio la uchaguzi , kabla ya kufungua kesi ya msingi (Mareva injunction), akiomba kusikilizwa upande mmoja (exparte) yaani yeye pekee bila  wajibu maombi.

Anadai kuwa Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi za TFF za Mwaka 2021, zinazotumika kuendesha uchaguzi huo ni batili.

Hivyo katika shauri jilo aliomba Mahakama iamuru uchaguzi huo usitishwe kusubiri afungue kesi ya msingi ili mahakama ijiridhishe na uhalali wa katiba na Kanuni hizo.

Hata hivyo Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Hussein Mtembwa imekataa kulisikiliza na mabadala yake imemuelekeza Wakili wake akiondoe mahakamani ikieleza kuwa haina mamlaka kulisikiliza.

Shauri hilo lilikuwa limepangwa kusikilizwa na Jaji Salma Maghimbi Jana  Ijumaa, Agosti 15 2025 sambamba na shauri lingine lenye maudhui kama hilo, lililokuwa limefunguliwa  la mawakili wanne. Hata hivyo mpaka saa 1:30 usiku alikuwa hajapata Jaji wa kulisikiliza.

Jaji Maghimbi aliyetarajiwa kulisikiliza baada ya kumaliza kuandika uamuzi wa pingamizi dhidi ya shauri la mawakili alipata dharura iliyomfanya akashindwa hata kusoma uamuzi huo badala yake ukasomwa na Naibu Msajili Livin Lyakinana.

Kutokana na dharura hiyo, Naibu Msajili Lyakinana alimpangia kwa Jaji mwingine ambaye hata hivyo hakuweza kupatikana mpaka saa 1:30 usiku.

Hivyo Naibu Msajili Lyakinana alimwelekeza aondoke tu lakini awe tayari wakati wowote kwani muda wowote hata usiku huo angeweza kuitwa na kusikilizwa kwa njia ya mtandao.

Hata hivyo shauri hilo limeitwa na Jaji Mtembwa  asubuhi ya leo kwa njia ya mtandao ambaye ameelekeza liondolewe bila kulisikiliza.

Wakili Nziku amesema kuwa baada ya kuitwa Jaji Mtembwa amesema kuwa shauri hilo lina mambo yanayofanana na shauri lingine lililoamuliwa Jana na kwamba kulingana na uamuzi huo wa jana basi hata hilo Mahakama haiwezi kulisikiliza.

“Kwa hiyo ameelekeza nili- withdraw (niliondoe mahakamani). Japo tulikuwa na hoja zetu za kisheria lakini hakutusikiliza, Kwa hiyo tumelazimika kuliondoa”, amesema Wakili Nziku na kuongeza:

Hata hivyo Wakili Nziku amesema kuwa suala hilo halijaisha na kwamba mteja wao amesema hajakata tamaa kwani ukiukwaji huo unaotokana na Katiba na Kanuni mbovu za TFF utaendelea

“Kwa hivyo sasa tunarudi mahakamani kwa njia nyingine. Sasa hatutafungua kesi ya kawaida ya madai bali sasa tunafungua kesi ya Kikatiba ili Mahakama iite na kukagua Katiba na Kanuni hizo za Uchaguzi kama zinakiuka Katiba”, amesema Wakili Nziku.

Kwa mujibu wa Wakili Nziku, tofauti na msimamo wa Mahakama kuwa migogoro dhidi ya TFF husikilizwa na vyombo vya ndani vya TFF, lakini kwa kesi za kikatiba hakuna chombo kingine chenye mamlaka ya kuisikiliza isipokuwa Mahakama Kuu peke.

Jaji Mtembwa katika uamuzi huo wa shauri la Mbingo amerejea uamuzi wa Jana katika shauri hilo lililokuwa limefunguliwa na mawakili Aloyce Komba, Jeremiah Mtobesya, Deusdedit Luteja na Denice Tumaini.

Katika shauri hilo, mawakili hao waliojitambulisha kuwa wapenzi na wadau wa soka, walikuwa wakiomba kibali cha kufungua shauri la mapitio pamoja na mambo mengine kupinga uhalali wa uchaguzi huo.

Jaji Maghimbi, katika uamuzi wake alilitupilia mbali baada ya kukubaliana na pingamizi lililowekwa na Wadhamini wa TFF, ambao walikuwa wajibu maombi wa pili, kuwa haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Jaji Maghimbi alikubaliana na hoja na mawakili wa TFF kuwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF ina vyombo byake yenyewe ambavyo ndivyo vyenye mamlaka ya kushughulikia migogoro/malalamiko kama hayo.