Mjumbe FIFA ampongeza Karia | Mwanaspoti

Mjumbe wa Baraza la Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Souleyman Waberi, amempongeza rais mteule wa TFF, Wallace Karia huku akiahidi kumpa ushirikiano mkubwa katika utawala wake madarakani.

Waberi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Djibouti, ametoa salama hizo katika mkutano mkuu wa TFF, unaofanyika leo jijini Tanga.

Akizungumza baada ya mkutano huo, Waberi amefurahishwa na jinsi uchaguzi huo ulivyofanyika huku akimtaja Karia mtu muhimu katika soka la Tanzania.

“Nimpongeze Karia kwa kutetea tena nafasi hiyo lakini niwapongeze pia wajumbe wote kwa imani kubwa ambayo mmeionyesha kwake,” amesema.

Aidha Waberi amesema, ataendelea kuunga mkono jitihada zote za soka la Tanzania ili kuhakikisha linapiga hatua na kuzidisha ushirikiano na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Karia aliyekuwa mgombea pekee wa urais katika kinyang’anyiro hicho, ameungwa mkono na wajumbe wote 76, waliokidhi vigezo vya kupiga kura.